Mavitu ya Hasheem Thabeet gumzo BDL

Muktasari:
- Lakini, mbali na ubora wa staa huyo aliyewahi kukipiga katika ile Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) ambako kuna mastaa kama LeBron James, Kelvin Durant, Giannis Antetokounmpo, Luka Doncic na wengineo, unaambiwa mashabiki wanaovijaza viwanja vya Donbosco, Upanga, Dar es Salaam wanamfuatilia zaidi mchezaji huyo.
UNAAMBIWA tayari Hasheem Thabeet, yule nyota wa kikapu wa kimataifa wa Tanzania anafanya vitu vyake katika michuano ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), lakini gumzo kubwa ni ubora anaouonyesha.
Lakini, mbali na ubora wa staa huyo aliyewahi kukipiga katika ile Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) ambako kuna mastaa kama LeBron James, Kelvin Durant, Giannis Antetokounmpo, Luka Doncic na wengineo, unaambiwa mashabiki wanaovijaza viwanja vya Donbosco, Upanga, Dar es Salaam wanamfuatilia zaidi mchezaji huyo.
Ni bahati iliyoje kwa timu ya Dar City iliyobahatika kumsajili kwa ajili ya mashindano hayo, kwani kila inapokuwa na mechi basi vile viwanja vinajaza mashabiki kushuhudia mavitu ya nyota huyo.
Unaambiwa kwamba kutokana na namna jamaa anavyodanki, kupokonya mipira na kushuti kelele majukwaani zinasindikiza vaibu hilo, ingawa hajacheza saaana kwani ndo kwanza mashindano hayo yameanza.
Thabeet ambaye kule NBA kazichezea timu za Memphis Grizzlies, Dakota Wizards, Houston Rockets na Oklahoma City Thunder amegeuka darasa kwa chipukizi na mastaa waliozoweleka katika mashindano ya BDL namna anavyozungusha katika dimba la kati akicheza kama 'centre'.
Katika mchezo dhidi ya Pazi, timu aliyowahi pia kuichezea Hasheem mchezaji huyo alionyesha ubora wa kipekee na kuisaidia kuondoka na ushindi wa pointi 62-47.
Ingawa kiwango alichoonyesha katika mchezo huo kinatajwa kuwa chini ya asilimia 20, lakini nyota huyo aliyewahi pia kukipiga katika ligi za Taiwan na Japan alionekana zaidi uwanjani akifanya vitu vyake na kuwafunika wachezaji wengine.
Wakizungumzia mambo anayoyafanya Hasheem, baadhi ya mashabiki walisema anaonyesha tofauti dhidi ya wachezaji wengine kutokana na kutumikia timu mbalimbali kubwa Marekani na Asia.
"Bado anafanya mambo makubwa kama kawaida yake. Ujue huyu ni mchezaji mkubwa na kacheza na nyota wakubwa duniani, hivyo hawezi kufanana na hawa tuliowazowea hapa kwetu," alisema Abdul Kaingu.
Naye Mwajabu Athuman alisema licha ya umri wa Hasheem kuanza kumtupa mkono, lakini bado anatisha kwani ubora na umahiri wake anaendelea kuuonyesha mchezoni.
"Umri kwake siyo tatizo, bado ni yuleyule sema kidogo kashuka, ila huwezi kumlinganisha na hawa wengine. Katika kikapu mchezaji anakuwa bora kadri anavyokua, angalieni mfano wa kina Lebron (James)," alisema.
Naye mchezaji wa Dar City, Amin Mkosa alisema mchezaji huyo anaipa heshima BDL kwa kucheza kana kwamba hana jina kubwa katika anga za kimataifa.
Mkosa ameliambia Mwanasposti kuwa heshima anayoitoa Hasheem BDL ni ile ya kujishusha kucheza katika mashindano kama hayo, ilhali alishavuka huko na sasa ni mchezaji wa kimataifa.
“Ni wachezaji wachache waliowahi kucheza Ligi ya NBA (ile ya Kikapu Marekani) wanaoweza wakashawishika kucheza ligi zao ndani,” alisema Mkosa.
Kwa mjibu wa Mkosa, alisema uchezaji anaocheza Hasheem ni kama asilimia 20 kutokana na ligi ilivyo sambamba na ushindani unaoonyeshwa na wachezaji wa timu zingine.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Pazi, Mkosa alisema uwezo mkubwa wa mchezaji mmojammoja ndiyo uliochangia kupata ushindi na kwamba, Hasheem alikuwa miongoni mwa waliobeba jahazi.
Hata hivyo, alikiri Pazi ina wachezaji wenye viwango bora kama timu zingine zinazoshiriki BDL.
Kocha msaidizi wa Pazi, Ramadhani Kalema alisema katika mchezo na Dar City, wapinzani wao walionekana bora kutokana na wingi wa mastaa.
Pazi katika BDL mwaka jana iliyoshika nafasi ya tisa, mwaka huu inaonekana kujipanga vizuri kutokana na usajili mkubwa ilioufanya unaohusisha nyota bora wa kikapu ukanda wa Afrika Mashariki.
UDSM VS WARRIORS
Pointi 24 zilizofungwa na UDSM Outsiders katika robo ya pili ya mchezo kati ya timu hizo ndizo zilizoifanya UDSM kuishinda Stein Warriors kwa pointi 69-65 katika mchezo uliopigwa Donbosco.
UDSM iliongoza kwa pointi saba katika robo ya pili, hali iliyofanya ipate pointi 24-10 hadi robo inamalizika. Kabla ya robo ya pili kuanza Warriors ilikuwa inaongoza kwa pointi 18-16 na ile ya tatu iliongoza kwa 19-16 huku ya nne ikivuna 17-14. Warriors iliyopanda daraja mwaka huu katika mchezo huo ilionyesha kiwango cha juu ambapo ulimshuhudia
Felix Mteba wa UDSM aliyeongoza kwa kufunga pointi 16 akifuatiwa na Mikado Ebengo aliyefunga 14.
Kwa upande wa Warriors alikuwa Jonas Mushi aliyefunga pointi 15 akifuatiwa na Brian Mramba aliyefunga pointi 13. Ushindi wa UDSM katika mchezo huo ni wa pili kushinda kwani katika mchezo wa kwanza iliifumua JKT kwa pointi 60-56.
CHUI VS KURASINI HEAT
Dharau na kujiamini kwa Kurasini Heat huenda ndivyo vilivyochangia ipoteze mchezo kwa kufungwa pointi 58-47 na Chui katika mchezo mwingine wa mashindano hayo.
Wachezaji wa Heat katika mchezo walionekana wakicheza taratibu kwa kujiamini, jambo ambalo kwa baadhi ya mashabiki waliokuwapo uwanjani lilitafsiriwa kuwa dharau dhidi ya Chui ambao ni wageni katika mashindano hayo.
Kurasini Heat iliyowahi kuwa bingwa mwaka 2020, ilianza mchezo taratibu robo ya kwanza ikiamini itapata matokeo mazuri, lakini ikajikuta ikigeuziwa kibao na Chui na kufungwa, kwani ilionekana kupoteza nafasi kila ilipozipata.
Chui inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ilianza kuongoza robo ya kwanza kwa pointi 11-7, ile ya pili Heat ikaongoza kwa pointi 12-11, huku ile ya tatu na nne Chui iliongoza kwa pointi 17-13 na 19-15 mtawalia.
DAKIKA 15 ZAIVUSHA REEL
Timu ya Reel Dream imekuwa ya kwanza katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kupata ushindi wa mezani kutokana na Kurasini Divas iliyokuwa ngeni kuvaa jezi nyeupe zilizofanana na wenyeji.
Mwamuzi wa mchezo huo, Enock Peter aliitaka Divas kubadili jezi kutokana na sheria na kanuni za mashindano hayo, lakini haikufanya hivyo.
Kwa mujibu wa kanuni, baada ya kuitaka timu hiyo ifanye hivyo aliipa dakika 15 ivae jezi zingine na baada ya muda kupita Reel iliitwa uwanjani na kupewa pointi mbili.
ROYALS, TRONCATTI TISHIO
Wakati Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam upande wa wanawake (WBDL), ikishika kasi imeonyesha Tausi Royals na DB Troncatti kuwa ndizo zinazoonekana kuwa tishio kutokana na ubora wa vikosi na vichapo vinavyotolewa dhidi ya timu pinzani.
Tausi Royals imeonyesha kwamba imejiandaa kufanya mambo makubwa mwaka huu, ambapo katika michezo miwili iliyocheza imeifumua Polisi kwa pointi 62-22 na kisha kuifunga Pazi Queens kwa pointi 68-46.
Nayo DB Troncatti katika mchezo wa kwanza iliishinda Polisi kwa pointi 77-58 kisha ikaifunga Reel Dream kwa pointi 67-47.
Hata hivyo licha ya timu hizo kuonekana kuwa bora, DB Lioness na Vijana Queens muunganiko wa vikosi vyake haujawa mzuri kama ilivyokuwa mwaka jana.
Lioness inayomtegemea Taundencia Katumbi, raia wa Kenya tofauti na Tausi Royals na DB Troncatti katika mchezo wa kwanza iliishinda Vijana Queens kwa pointi 46-38 huku ule wa pili ikiifunga Kigamboni Queens kwa pointi 81-39.