Maujanja ya Yanga yanavyoitesa Simba

Muktasari:

  • Mafanikio ya Simba hadi sasa kwa msimu huu ni kushinda Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano. Michuano yote hiyo imeshirikisha timu nne. Ngao ya Jamii kulikuwa na Yanga, Azam, Singida Fountain Gate na Simba wenyewe. Kombe la Muungano zilishiriki KMKM na KVZ kutoka Zanzibar na Tanzania Bara zilikuwa Azam na Simba.

SIMBA SC inapambana kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Simba imeukosa ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa tatu mfululizo. Simba imeishia tena robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba imeishia hatua ya 16 bora katika Kombe la Shirikisho (FA).

Mafanikio ya Simba hadi sasa kwa msimu huu ni kushinda Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano. Michuano yote hiyo imeshirikisha timu nne. Ngao ya Jamii kulikuwa na Yanga, Azam, Singida Fountain Gate na Simba wenyewe. Kombe la Muungano zilishiriki KMKM na KVZ kutoka Zanzibar na Tanzania Bara zilikuwa Azam na Simba.

Kumekuwa na kelele nyingi za mashabiki na wanachama wa Simba juu ya mwenendo wa timu hiyo msimu huu, huku wakiilinganisha na Yanga.

Tunawaelewa mashabiki na wanachama wa Simba wanachopitia kwa sasa kutokana na mwenendo wa timu hiyo, hii inatokana na namna mazuri yaliyokuwepo kwa misimu takribani minne hapo kabla kuanzia 2017-2018 hadi 2020-2021.

Katika soka la Tanzania, ukizungumzia timu tishio kwenye michuano ya kimataifa kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni Simba ndio itahusika, lakini sasa imeshindwa kuwa na muendelezo sahihi.

Yanga ambayo ilikuwa haina mwenendo mzuri katika michuano ya kimataifa, viongozi wake walikaa chini na kuangaliaa awali walikuwa wanakosea, wakaja na njia sahihi ya kupita, ghafla wameanza kuuona mwanga.

Msimu wa 2022-2023 Yanga ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikaweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kucheza hatua hiyo tangu kuasisiwa kwa michuano hiyo mwaka 2004.

Msimu huu 2023-2024 Yanga imecheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1935, lakini pia ilifuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu ilivyofanya hivyo takribani miaka 25 iliyopita.

Hayo yote yametokea ndani ya kipindi cha muda mfupi wakati viongozi wa timu hiyo walipokubali kukaa chini na kuangalia wapi walikuwa wanakosea, sasa matunda yanaonekana.

Hiki wanachopitia Yanga kwa sasa kilele cha furaha, Simba walikuwa nacho misimu kadhaa nyuma, lakini ni kama walisahau wafanye nini kwenda mbele zaidi.

Matokeo yake hivi sasa wameanza kuonana wabaya kila kukicha huku mambo kadhaa yakiibuliwa ambapo yote hayo viongozi hawakwepi lawama.

Wakati Simba ilipokuwa kwenye ubora wake na kutishia vigogo wa soka Afrika, walikuwa na wachezaji wenye uwezo wa kuamua matokeo muda wowote.

Clatous Chama, Luis Miquisone wakiwa kwenye ubora wao walifanya watakavyo, bila ya kusahau uwepo wa Aishi Manula golini, Mohammed Hussein na Shomari Kapombr katika mbavu mbili za ulinzi, kushoto na kulia. 'Fisrt Eleven' ya Simba ilikuwa moto.

Viongozi ni kama walibweteka, wakasahau kwamba kuna muda viwango vya wachezaji hushuka kutokana na kutumika sana, hivyo warithi wao walishindwa kuandaliwa mapema na hata waliposajiliwa wengine hawakuwa kama wale.

Chama na Luis wakauzwa baada ya vigogo wa soka Afrika kuridhishwa na viwango vyao, Simba ikaingia sokoni kusaka mbadala wake, lakini mpaka leo haijawapata, ikaamua kuwarudisha kundini nyota hao. Wamerejea lakini sio kama wale waliokuwa mwanzo, wameshuka viwango.

Ukiangalia kwa asilimia kubwa kikosi cha Simba kilichokuwa bora na tishio kwa misimu minne mfululizo wachezaji waliobaki ni kama wamechoka na wanaendelea kutumika huku wakikosa mbadala wao sahihi.

Hii imetokana na usajili unaoendelea kufanyika ndani ya timu hiyo haukidhi matakwa kwani hata makocha waliopita wamekuwa mashahidi wa hilo.

Roberto Oliveira na Abdelhak Benchikha, ni makocha wawili walioifundisha Simba msimu huu na kuondolewa wote kwa kushindwa kuirudisha timu kwenye ushindani kama zamani huku kilio cha makocha hao ni aina ya usajili uliofanyika hauendani na ubora walioutaka.

Tunakwenda kuumaliza msimu wa 2023-2024, kinakuja kipindi cha usajili ambacho Simba wanapaswa kuwa makini wasirudie makosa yaleyale.

Tumeona dirisha dogo msimu huu wamewaondoa Moses Phiri na Jean Baleke kwenye eneo la ushambuliaji, wamekuja Pa Omar Jobe na Freddy Michael Koublan ambao kila Mwanasimba ameonekana kutoridhishwa na hilo.

Baleke tangu ameondoka Simba Januari mwaka huu, juzi tu ndiyo amepitwa mabao kwani alikuwa kinara wa ufungaji kikosini hapo katika ligi kuu akifunga nane. Hii inafikirisha na kuonyesha kwamba walioletwa kuchukua nafasi zao wameshindwa kuifanya kazi ipasavyo.

Kumekuwa na msemo kwamba usajili ni kama kamari, hilo linaweza kuingia akilini kwani hata Yanga wanaotamba kwa sasa kuna wachezaji wamewaleta na kushindwa akiwemo Hafiz Konkoni ingawa wengine wametoboa.

Hivyo basi, Simba inahitaji kuongeza umakini katika usajili ujao, kwani waliwezaje kipindi kile wakaitikisa Afrika na sasa wanashindwa nini.

Kama kuna mtu ndiye mtaalamu wa hayo mambo na sasa hayupo basi hakuna budi kumrudisha ili iwe faida kwa klabu kwani tunaamini kwamba kinachojengwa hapa ni heshima ya klabu na si mtu binafsi.

Kama kauli mbiu yenu inavyosema Simba Nguvu Moja, basi tuione hiyo nguvu ikiwa na umoja kama zamani. Isiwe mnaishi katika kauli mbiu ya Nguvu Moja huku nyuma ya pazia kila mtu ana nguvu yake.


WASIKIE WADAU

Fowadi wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel anaamini bado timu hiyo inawachezaji wenye uwezo wa kufanya makubwa, kikubwa ni kuaminiwa wale ambao wamepewa nafasi mwishoni mwa msimu na wamenoyesha makali yao ili kuongeza kitu cha tofauti.

"Hawa wakina Chasambi, Balua ni wachezaji wazuri wanatakiwa kuendelea kuaminiwa, sio mbaya kuongeza wachezaji wawili hadi watatu ambao ubora wao utakuwa mkubwa na sio kusajili wachezaji ambao watashindwa kuonyesha utofauti na waliopita," alisema.

Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr amewashauri waajiri wake hao wa zamani kuwa makini katika kipindi hiki cha usajili ili kuongeza wachezaji wa maana ambao wataongeza nguvu kwenye kikosi chao ili kurejesha heshima yao katika ligi.

"Nadhani viongozi wa Simba wanatakiwa kuwa macho ni bora kuwa na muda mrefu katika ufuatiliaji au ukasajili wachezaji watatu au wanne ambao watakuwa na mchango mkubwa kuliko kuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao watafanya mambo ya kawaidi," alisema kocha huyo Muingereza.

Naye nyota wa zamani wa Yanga, Credo Mwaipopo anaamini Simba inahitaji majina mapya matatu yenye ubora zaidi ya wachezaji walipo, wakifanya hivyo wataongeza kitu kwenye timu na sio ajabu msimu ujao wakafanya makubwa katika ligi na kimataifa.

"Ukiitazama Simba sio kwamba ni timu mbovu sana, hapana wanatakiwa kukiboresha tu kikosi chao kwa kusajili wachezaji wa nguvu, wakifanikiwa katika hilo kitakachobaki ni kujenga tu timu kitu ambacho hakiwezi kuchukua muda mrefu sana," alisema.