Maua Sama: Familia ilikataa nisifanye muziki kisa iokote

Muktasari:
Maua Septemba 17, 2018 alishikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma ya kosa la huharibifu wa mali kwa kurusha pesa kisha watu kuonekana kuzikanyagakanya katika video ya wimbo wake wa iokote
Dar es Salaam. Mwanamuziki Maua Sama baada ya kuachia wimbo wa 'Niteke', amesema familia yake ilikataa asifanye muziki kabisa.
Maua aliyetamba na nyimbo 'iokote', 'nakuelewa' ameiambia MCL Digital jana Septemba 2, 2019 kuwa baada ya kupata matatizo ya kuwekwa rumande alihitaji kupata mapumziko kufanya muziki ila familia yake ilikataa asiendelee kabisa.
"Wimbo wa iokote ilitakiwa kuwa ni wimbo wa mwisho kwangu katika kufanya muziki, kwani kutokana na ishu ya kuwekwa rumande wazazi wangu hawakutaka niendelee na muziki japo mimi mwenyewe nilitaka kupumzika tu kwa muda," alisema Maua.
Maua alisema ilibidi akae chini na familia yake na kuweka sawa suala la yeye kuendelea na muziki na baada ya kuelewana nao ndipo alipoamua kutoa wimbo wake mpya wa Niteke.
"Baada ya kutoa wimbo huu sasa nafikiria kutoa wimbo utakaohusu changamoto nilizopitia kwani tukio la kuwekwa rumande halitaweza kufutika kichwani mwangu," alisema.
Maua Septemba 17, 2018 alishikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma ya kosa la huharibifu wa mali kwa kurusha pesa kisha watu kuonekana kuzikanyagakanya katika video ya wimbo wake wa iokote.