Matajiri Simba wafunga bao la mkono

Mshambuliaji wa Azam Brian Majegwa (kulia) akifanya mambo yake.
Muktasari:
WACHAMBUZI wa soka wa Tanzania wamesikia usajili wa nyota wa Uganda, Brian Majwega, kwenda Simba na wakatamka kwamba vigogo waliokamilisha zoezi hilo wamepiga goli la mkono. Mchezaji huyo ataonekana katika mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara ambapo kwa kutumia vidole vyake vitano vya mkono wa kulia, ameiandikia Simba barua kuomba kuichezea ili kulinda kiwango chake na nakala ya barua hiyo imetumwa pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
WACHAMBUZI wa soka wa Tanzania wamesikia usajili wa nyota wa Uganda, Brian Majwega, kwenda Simba na wakatamka kwamba vigogo waliokamilisha zoezi hilo wamepiga goli la mkono. Mchezaji huyo ataonekana katika mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara ambapo kwa kutumia vidole vyake vitano vya mkono wa kulia, ameiandikia Simba barua kuomba kuichezea ili kulinda kiwango chake na nakala ya barua hiyo imetumwa pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Nyota huyo ana mgogoro wa kimkataba na timu yake ya Azam.
Majwega alipotua Azam tu katikati ya msimu uliopita, aliibuka nyota katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo katika mechi nne alitengeneza nafasi tano zilizoa mabao kabla ya baadaye kufanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu.
Mara baada ya kupata taarifa za usajili wake jana Alhamisi jioni, kocha wa Simba, Dylan Kerr, alifanya mawasiliano ya moja kwa moja na kocha wa timun ya taufa ya Kenya, Bobby Williamson ili kufahamu uwezo wa nyota huyo ambapo kocha huyo alimtoa mashaka na kumwambia jamaa ni jembe, piga naye kazi.
Bobby aliwahi kumfundisha nyota huyo wakati anaifundisha timu ya taifa ya Uganda ‘The cranes’ mwaka 2008-13.
Kocha mzawa, Kennedy Mwaisabula, alisema kama Kerr atampa Majwega nafasi katika moja ya winga zake, ataukubali mziki kwani mchezaji huyo ana kasi, anapiga chenga na pasi za maana.
“Majwega akicheza na washambuliaji wepesi kama Hamis Kiiza na Ajibu (Ibrahim), wataweza kufunga sana, ana kasi na anaingia, kocha tu akubali kumpa nafasi na kupunguza idadi ya viungo,” alisema Mwaisabula.
Kocha mwingine, Joseph Kanakamfumu, alisema Simba imelamba dume kumsajili winga huyo huku akihoji ilikuwaje nyota huyo akaondoka Azam wakati alikuwa miongoni mwa wachezaji tishio.
“Simba inamhitaji sana Majwega kwa sasa, kama kocha atampa nafasi ataona mambo, ana uwezo binafsi wa kukaa na mpira, anaweza pia kucheza nyuma ya straika na kutoa pasi za maana,” alisema Kanakamfumu ambaye alifananisha ujio wake Simba kama ulivyokuwa wa marehemu Patrick Mafisango aliyekuwa ameondoka Azam katika mazingira kama hayo na baadaye kutamba na Simba.
Mmoja wa mabosi wa Azam alikiri kuwa usajili huo wa Majwega ni mkubwa kwa Simba kwani nyota huo aliondoka Azam akiwa katika kiwango bora na hakustahili kutemwa.
“Aliondoka kutokana na sababu fulani fulani za kisiasa, lakini ni mchezaji mzuri mno, mpaka leo hata sielewi ilikuwaje,” alisema.
SIMBA YATUA BURUNDI, ETHIOPIA
Taarifa nyingine za usajili zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana ni kwamba kiongozi mmoja wa juu wa Simba anatazamiwa kwenda Burundi ili kumaliza utata wa usajili wa straika, Laudit Mavugo na kuangalia uwezekano wa kumsajili pia Kelvin Ndayisenga ambaye tayari alishaivutia Simba.
Hata hivyo ujio wa straika Doumbie Ernest kutoka Cameroon unaweza kutibua mpango huo endapo atafanya vizuri katika mazoezi.
Bosi huyo pia anatarajiwa kwenda Ethiopia kufuatilia vipaji katika Kombe la Chalenji.