KMKM mabingwa wapya Kombe la FA Zanzibar

Muktasari:
- Kipigo hicho kimeifanya Chipukizi kutoka kisiwani Pemba kushindwa kutetea taji lake usiku wa leo na kukosa fursa ya kuiwakilisha Zanzibar kimataifa msimu ujao.
TIMU ya KMKM imetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) baada ya kuichakaza Chipukizi mabao 4-2 katika mchezo wa fainali uliochezwa leo Juni 21, 2025 kwenye Uwanja wa Mao Zedong uliopo Mjini Unguja.
Kipigo hicho kimeifanya Chipukizi kutoka kisiwani Pemba kushindwa kutetea taji lake usiku wa leo na kukosa fursa ya kuiwakilisha Zanzibar kimataifa msimu ujao.
Mchezo huo uliochezwa kuanzia saa 1:00 usiku, uliokuwa na presha ya kila mmoja kuhitaji kushinda lakini dakika 90 zimeamua KMKM kuibuka kidedea.
Mchezaji wa KMKM, Jasper Yaw aliweka kimiani bao la kwanza dakika ya 15 huku Haji Makame akiongeza la pili, kabla ya Faki Mwalimu kuifungia Chipukizi dakika ya 38 na kufanya dakika 45 za kipindi cha kwanza cha mchezo huo kumalizika kwa KMKM kuongoza kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili, Haji Makame aliongeza bao la tatu kwa KMKM kisha Abrahman Othman akahitimisha la nne.
Abdallah Nassor aliweka la pili la Chipukizi dakika ya 89 na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa mabao 4-2.
Mabingwa hao wapya wa Kombe la FA, wataiwakilisha Zanzibar katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, huku timu ya Mlandege ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar.