Mastaa wazawa Azam FC wafunika

Muktasari:
- Yakifungwa mabao 521 hadi sasa msimu huu, wachezaji wazawa wamefunga 280 huku Azam FC ikiongoza kwa nyota wa timu hiyo kufunga mabao 28, ikiwa ni idadi kubwa zaidi tofauti na kwa wapinzani wao wakubwa hapa nchini Yanga na Simba.
WAKATI Ligi Kuu Bara ikienda ukingoni msimu huu wa 2024-2025, tayari jumla ya mabao 521, yamefungwa ikiwa ni idadi kubwa zaidi tofauti na ya msimu uliopita ambao yalifungwa 517, ikionyesha kasi ya ufungaji imeongezeka kwa mastaa mbalimbali.
Yakifungwa mabao 521 hadi sasa msimu huu, wachezaji wazawa wamefunga 280 huku Azam FC ikiongoza kwa nyota wa timu hiyo kufunga mabao 28, ikiwa ni idadi kubwa zaidi tofauti na kwa wapinzani wao wakubwa hapa nchini Yanga na Simba.
Katika mabao 521 yaliyofungwa, 280 yamefungwa na wachezaji wazawa, 224 yamefungwa na wageni huku mengine 17 yakiwa ni ya kujifunga, ambapo mbali na Azam FC inayoongoza timu nyingine inayofuatia ni maafande wa Mashujaa FC waliofunga mabao 27.
Kwa upande wa Yanga inayoongoza Ligi Kuu Bara kwa pointi 73, katika mabao 71, iliyofunga ni 21 yaliyofungwa na wachezaji wazawa, huku Simba iliyo ya pili kwa pointi 69, kwenye mabao 62 iliyoyafunga, ni 14, tu ndio yaliyofungwa na nyota wa kizawa.
Nyota wa maafande wa JKT Tanzania wamefunga mabao 24, ikifuatiwa na Dodoma Jiji iliyofunga 22, sawa na Tanzania Prisons, huku Fountain Gate ikifunga 21 kama ilivyokuwa pia kwa Yanga, wakati kwa KenGold na KMC FC kila moja imefunga mabao 20.
Kikosi cha ‘Wauaji wa Kusini, Namungo FC wachezaji wazawa wamefunga mabao 17, kati ya 23 iliyofunga hadi sasa, huku kwa upande wa Coastal Union imefunga 14, sawa na yaliyofungwa na Simba, huku Kagera Sugar iliyoshuka daraja ikifunga 11.
Wachezaji wa Tabora United wamefunga mabao tisa, wakifuatiwa na Pamba Jiji iliyofunga manane, huku Singida Black Stars iliyo nafasi ya nne kwa pointi 53, ndio timu inayoongoza kwa wazawa kufunga mabao machache zaidi ambayo ni mawili tu.