Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Masikini Tambwe! Ugonjwa usiojulikana wamtesa

Dar es Salaam. Mungu ameniponya. Hiyo ni kauli ya mchezaji wa Yanga, Amiss Tambwe aliyotoa akieleza matatizo yaliyomkuta katika medani ya soka.

Mfungaji huyo bora matatu wa Ligi Kuu Bara, alitoa kauli hiyo alipokuwa akieleza ugonjwa usiojulikana  unaomsababishia maumivu makali ya goti yaliyomuweka nje ya uwanja tangu kuanza msimu huu.

Hata hivyo, mtaalamu wa magonjwa ya viungo Mwanandi Mwankemwa, alisema pamoja na majeraha yanayotokana na sababu mbalimbali, lakini suala la saikolojia limekuwa likiwasumbua baadhi ya wachezaji wanapopata maumivu.

Tambwe alisema maumivu ya goti yanatishia ajira yake Yanga, baada ya kushindwa kucheza katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Akizungumza Dar es Salaam, Tambwe alisema anapitia kipindi kigumu katika maisha ya soka, lakini ana amini Mungu amemponya baada ya madaktari kushindwa kubaini ugonjwa unaomsumbua.

Tambwe alidokeza baada ya kuhangaika muda mrefu katika hospitali tofauti na kufanyiwa upasuaji wa goti bila mafanikio, alimgeukia Mungu kufanya maombi.

Mshambuliaji huyo alisema alianza kupata maumivu ya goti la mguu wa kushoto akiwa kambini Zanzibar  walipokuwa katika maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu.

"Nimehangaika hospitali muda mrefu madaktari hawakuona tatizo, wakati mwingine nilikuwa sipati maumivu nikiwa nyumbani, lakini nikirejea kambini na kuanza mazoezi tu hali inabadilika,”alisema Tambwe.

Mchezaji huyo wa zamani wa Simba, alisema kutokana na maumivu makali aliyokuwa akipata, alifanyiwa upasuaji wa goti, lakini hakuonekana na tatizo.

"Madaktari waliniambia nipumzike hawakuona tatizo nilikuwa napata maumivu makali nilipokuwa najiona niko sawa nikijaribu kucheza goti lilikuwa linavimba," alisema mshambuliaji huyo.

Mshambuliaji huyo alisema baada majibu ya madaktari kuhusu upasuaji, aliamua kutafuta njia nyingine ya kuanza maombi kwa Mungu ambaye kwa mujibu wa maelezo yake anadai amemponya.

"Kocha Mwandila (Noel) alinipa programu maalumu ya mazoezi ambayo naimaliza wiki hii baada ya hapo ataniambia nini cha kufanya kama ni kujiunga na wenzangu au vipi lakini kimsingi kwa sasa najiona niko fiti,"alisema Tambwe.

Hata hivyo, Tambwe alisema licha ya kuwa nje ya uwanja muda mrefu, nafasi yake ilijazwa vyema na wachezaji wengine aliodai waliitendea haki katika mashindano mbalimbali.

Kauli ya Daktari

Licha ya daktari wa Yanga, Edward Bavu kudai Tambwe ana tatizo hilo, Mwanandi Mwankemwa ametaja sababu tatu zinazochangia mchezaji kupata majeraha ya goti.

Daktari huyo aliyebobea katika tiba ya magonjwa ya viungo, alisema pamoja na mchezaji kuathirika kisaikolojia anapopata jeraha, lakini kucheza mechi ngumu mfululizo bila kupata muda mzuri wa kumpumzika kunachangia kupata maumivu.

Mwankemwa ambaye ni daktari wa timu ya Azam, alisema mchezaji anapocheza muda mrefu bila kupumzika ni rahisi kupata jeraha kwa kuwa viungo vimetumika zaidi kupita uwezo wake.

Pia, daktari huyo alisema umri mkubwa kwa wachezaji ni miongoni mwa sababu zinazochangia mchezaji kukaa nje kwa miezi sita hadi tisa anapopata majeraha ya viungo.

Mwankemwa alidokeza ubovu wa viwanja vinavyotumika vinachangia mchezaji kupata majeraha ya mara kwa mara.