Mashujaa yaiota nne Bora mapemaa!

Muktasari:
- Timu hiyo itakayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa pili mfululizo, ikitoka kumaliza nafasi ya nane, katika dirisha kubwa la usajili linalendelea tayari imeshusha majembe mapya saba, Carlos Protus, Ally Nassoro Iddi ‘Ufudu’, Mohamed Mussa, Mathew Michael, Ismail Mgunda, Robert Mathias na Yusuph Dunia, huku ikiachana na nyota wake tisa.
WAKATI kikosi cha Mashujaa Kigoma kikiendelea kujifua kwa kupiga tizi la nguvu katika fukwe za bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam, uongozi wa timu hiyo umesema malengo ya msimu huu ni kumaliza katika nafasi nne za juu katika Ligi Kuu Bara ili ikate tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.
Timu hiyo itakayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa pili mfululizo, ikitoka kumaliza nafasi ya nane, katika dirisha kubwa la usajili linalendelea tayari imeshusha majembe mapya saba, Carlos Protus, Ally Nassoro Iddi ‘Ufudu’, Mohamed Mussa, Mathew Michael, Ismail Mgunda, Robert Mathias na Yusuph Dunia, huku ikiachana na nyota wake tisa.
Mtendaji Mkuu wa Mashujaa, Benson Mwangatwa aliliambia Mwanaspoti, kuwa, baada ya kutimiza lengo la kuibakisha timu msimu uliopita, safari hii wanakuja kivingine na watashangaza watu kwani wamedhamiria kufanya makubwa ili kukata tiketi ya CAF kama ilivyozipata Simba, Yanga, Azam na Coastal Union.
Alisema usajili wanafanya na maandalizi makubwa wanayoendelea kuyafanya katika kambi yao jijini Dar es Salaam wana matumaini makubwa ya kufikia malengo yao msimu ujao wa mwaka 2024/2025 ambao utaanza Agosti 16, mwaka huu.
“Sisi tunafanya usajili kwa malengo kwa sababu mwaka jana tulikuwa na malengo ya kupanda na kusalia Ligi Kuu, jambo ambalo tumefanikiwa na tumeendelea kuwashangaza wengi kwahiyo usajili wa mwaka huu tunataka tuwe na fikra za kimataifa,” alisema Mwangatwa
Akizungumzia suala la usajili kwenye klabu hiyo alisema bado unaendelea kwani kuna wachezaji wapya watatambulishwa muda wowote, huku akiwaahidi mashabiki kuwa bado vyuma hatari vitashuka katika kukiunda kikosi hicho chini ya Kocha wao, Mohamed Abdallah ‘Baresi’.
“Tunaendelea kufanya usajili na vyuma vinakuja na wapo wachezaji wazuri wametoka katika klabu zenye majina makubwa lakini mtegemee usajili wa Mashujaa ni mzuri kwa sababu tumejiandaa ili tuweze kushiriki kikamilifu na ili tushike nafasi za juu na kushiriki mashindano ya kimataifa,” alisema