Mashabiki Yanga wafanya usafi Polisi

WANACHAMA na mashabiki wa Klabu ya Yanga tawi la Kubwa Kuliko Morombo jijini Arusha wamezindua wiki ya Wananchi kwa staili ya aina yake baada ya kufanya usafi katika kituo cha Polisi Morombo.
Wiki ya Wananchi ni maalum kwa Yanga kutambulisha kikosi chao kipya ambacho watatumia kwenye mashindano ya ndani na ya kimataifa kwa mashabiki ambapo kabla ya kilele timu hiyo kupitia wanachama na mashabiki wake nchi nzima imekuwa na desturi ya kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji.
Shangwe na shamra shamra ziliuteka eneo hilo ambapo misafara ya wanachama kuzunguka kufanya usafi ambapo baadae pia waliamua kupiga msasa soko la Morombo kabla ya kuitimisha katika eneo la tawi lao huku wakishangilia kwa staili ya kutetema kama mshabuliaji wao Fiston Mayele.
Makamu mwenyekiti wa tawi la Yanga kubwa kuliko Morombo, Khalfani Msangi anasema kama ilivyo kawaida yao kurudisha kwa jamii waliamua kufanya usafi katika maeneo hayo huku akiongeza kuwa bado wataendelea na shughuli kama hiyo ambapo kesho Ijumaa wataenda kutoa misaada katika kituo cha kulelea watoto yatima eneo la Murieti.
“Mwitikio ulikuwa mkubwa wanayanga wamejitokeza kwa wingi na hii inaoshesha moja kwa moja tunaunga mkono kuelekea siku yenyewe ambayo ni jumamosi na tunashukuru waliojitokeza na zoezi hili tutaendelea nalo na sasa tumepanga kwenda jijini Dar es salaam kushuhudia mchezo kati ya Yanga dhidi ya Vipers FC”. alisema Ngollo.
Anasema kutokana na usajili ambao timu hiyo imefanya hawana wasiwasi hata kidogo kwani anaamini watabeba tena makombe yote matatu ya ndani kwa maana ya ngao ya jamii, ubingwa wa Ligi na kombe la Shirikisho Azam (ASFC) lakini pia kufanya vizuri klabu bingwa Afrika.
Victor Vicent anasema anajivunia kuwa mwana Yanga huku akisifia usajili ambao umefanywa na timu hiyo msimu huu anaoamini utawafanya kuendelea kutesa lakini kupata mafanikio makubwa kimataifa.
"Tunaimani na uongozi hadi wachezaji yani una Aziz Ki alafu timu ambayo imesajili sajili tu ukufunge waje na kalamu na daftari jumamosi taifa waone tunafundisha soka". alisema Victor.
Kwa upande wake shabiki mwingine Loveness Chami anasema anachojivunia ni kuona wapinzani wao wataendelea kuteseka kutokana na nama timu yao ilivyo kwa sasa ambayo kila mmoja wao anaringa na kujivunia usajili mzuri uliofanywa na uongozi.