Mashabiki kiduchu waingia Jamhuri kuwashudia JKT, Yanga

Muktasari:
Mchezo huu unachezwa kwenye uwanja wa Jamhuri, Dodoma
Dodoma. Wakati mchezo ukianza hapa uwanjani Jamhuri, hamasa ya mashabiki walioingia uwanjani haijawa kubwa.
Licha ya Yanga kuwa na mashabiki wengi kama ilivyo Simba, lakini haijawa sababu ya mashabiki kufurika ndani ya uwanja kama ilivyotarajiwa.
Hapa uwanjani, sehemu kubwa ya majukwaa haswa ya mzunguko, haina mashabiki wengi jambo linaloonesha kwamba mashabiki wengi hawajaona umuhimu wa kufika uwanjani leo.
Imezoeleka siku zote kwenye mechi zinazohusu timu za Yanga na Simba, uwanja wa Jamhuri hufurika mashabiki. Lakini leo hali ni tofauti ukilinganisha na mechi zilizopita za Simba.
Simba ilipocheza mechi zake mbili kwenye uwanja huu dhidi ya JKT Tanzania na Dodoma Jiji, sehemu kubwa za uwanja huu zilijaa tofauti na leo.
Jukwaa pekee ambalo limefurika mashabiki ni lile la upande wa pili linalotazamana na jukwaa kuu, pamoja na kiasi chake kwenye majukwaa ya kulia na kushoto mwa jukwaa kuu.
Viingilio vya jukwaa kuu vimeuzwa kwa Sh.20,000 wakati majukwaa ya VIP B ni Sh. 10,000 na V.I.P C ni Sh. 15, 000.
Hawa hapa waamuzi wanaoamua mchezo huu
MWAMUZI Ahmada Simba kutokea mkoani Mwanza, ndiye anayeongoza waamuzi wenzake watatu kuamua mchezo huo.
Ahmada, mwamuzi mzoefu anasaidiwa na Frednand Chacha pia kutokea Mwanza, pamoja na Sikudhani Mkurungwa kutoka mkoani Njombe.
Waamuzi hao wana kazi ya ziada kuhakikisha wanachezesha mchezo huu bila kukosea kufuatia malalamiko ya timu ya Yanga kwenye mchezo uliopita wa suluhu dhidi ya Namungo mkoani Lindi.
Mbali na waamuzi hao, mwamuzi wa akiba ni Florentina Zablon wa Dodoma, wakati kamisaa wa mchezo ni Alanus Iwena kutokea Mwanza.
Timu zote mbili zinasaka matokeo ya ushindi kwenye mchezo huu ili kujiweka kwenye nafasi mbili tofauti.
Wakati JKT Tanzania wakijaribu kushinda ili kukimbia hatari ya kushuka daraja, Yanga wao wanajaribu kutaka kuisimamisha Simba kubeba ubingwa wa nne mfululizo.
Imeandikwa na Matereka Jalilu