Kipa Berkane aichimba mkwara Simba

Muktasari:
- Simba na RS Berkane zinarudiana Jumapili katika mechi ambayo inatarajiwa kuwa ngumu ikizingatiwa kwamba hii ni mara ya pili kwa Simba katika kipindi cha miaka 31 kutinga hatua ya fainali ya mashindano ya klabu Afrika.
KIPA wa RS Berkane ya Morocco, Munir El Kajoui amesema kikosi chao kimetua Tanzania kwa kazi moja tu - kuhakikisha kinakamilisha kile walichokianza kwenye mechi ya kwanza ya fainali dhidi ya Simba SC wikiendi iliyopita, nchini kwao.
Akizungumza kabla ya mazoezi leo, Ijumaa, ikiwa ni siku moja baada ya kikosi hicho kuwasili Zanzibar kwa ajili ya mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Munir amesema: “Tunafahamu Simba ni timu kubwa, wanapambana mpaka mwisho. Lakini, tumeshikamana kama familia. Tupo tayari kwa lolote. Tumekuja hapa kumaliza kazi tuliyoianza Berkane.”
Munir ambaye ni miongoni mwa wachezaji wazoefu wa Berkane amesema kuwa siri ya mafanikio ya kikosi chao ni mshikamano na nidhamu.
"Katika klabu yetu kila mmoja anajua majukumu yake. Tunaongozwa na nidhamu, heshima na mshikamano. Hatuna mastaa wakubwa, bali tuna timu yenye mshikamano mkubwa,” amesema.
Kuhusu mechi ya marudiano Jumapili ambapo wapo mbele kwa mabao 2-0 waliyoyapata Morocco, Munir amesema: “Tutacheza kwa akili na umakini mkubwa. Tunajua presha ya ugenini ilivyo, lakini sisi pia tumejiandaa kwa hilo. Hatutabweteka na ushindi wa kwanza.”
Akizungumzia mashabiki wa RS Berkane waliopo nyumbani kwao kipa huyo amesema kwamba wanawaamini na wamewapa moyo kuja kupambana ili wabebe ubingwa wa Shirikisho.
“Wanatuamini. Wametupa moyo. Sasa ni zamu yetu kuwarudishia kwa kupeleka kombe nyumbani. Tuna deni kwao,” amesema.
Simba na RS Berkane zinarudiana Jumapili katika mechi ambayo inatarajiwa kuwa ngumu ikizingatiwa kwamba hii ni mara ya pili kwa Simba katika kipindi cha miaka 31 kutinga hatua ya fainali ya mashindano ya klabu Afrika.