Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yatia mguu ishu ya kuingia bure mechi ya Simba,  Berkane

BURE Pict

Muktasari:

  • Kauli hiyo imekuja baada ya kusambaa taarifa tangu jana Mei 22, 2025 na leo zikidai Rais Hussein Mwinyi amelipia gharama zote hivyo wananchi wataingia bure kutazama mechi hiyo.

Baada ya kuibuka taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikidai Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amelipia gharama zote za mechi ya marudio ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na RS Berkane ya Morocco, serikali imesema viingilio vipo pale pale.

Mechi hiyo ya marudio inatarajiwa kuchezwa Jumapili Mei 25, 2025 saa 10: 00 jioni katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Jana Mei 22, 2025  zilianza kusambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikihamasiaha wananchi kujitokeza kwa wingi kwani tayari Rais Mwinyi amelipia gharama zote na wananchi wataingia bure kushuhudia mchezo huo.

Akifafanua jambo hilo wakati akizungumza na vyombo vya habari leo Mei 23, 2025 Kamishna wa Idara ya Michezo katika Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo Zanzibar, Ameir Mohammed Makame amesema alicholipia Rais ni gharama za uwanja asilimia 15  na siyo viingilio.

“Hizi taarifa jamani sio za kweli kwamba mheshimiwa Rais amelipia gharama zote na viingilio. Tunaomba ieleweke kwamba alichosaidia kwa mapenzi makubwa aliyonayo amelipia asilimia 15 tu za uwanja. Kwa hiyo viingilio vipo pale pale,” amesema.

Kuna aina tatu za viingilio katika mchezo huo ambapo daraja la kwanza (VIP) ni Sh50, 000,  pili Sh30,000 na Sh10,000 kwa daraja la tatu.

Naye Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amesema kupitia Kamisheni ya Utalii watatumia fursa hiyo kuitangaza Zanzibar ikizingatiwa michezo kwa sasa ni moja ya bidhaa inayotumika kuitangaza Zanzibar na watatumia bidhaa mpya ya Visit Zanzibar kuinadi.

“Hii ni sehemu ya kuitangaza Zanzibar kitaifa, kikanda na kimataifa na tutatumia fursa hiyo kujitangaza na maana mechi hii itakuwa inatazamwa na zaidi ya mataifa 27 ya Afrika,” amesema

Kwa mujibu wa Soraga, watalii wengi wanaokwenda kutembelea Zanzibar wanatoka Ulaya, lakini huo ni mpango mpya kuongeza watalii kutoka Afrika.

“Nasema hivi kwa sababu Morocco wamekuja na watu wengi sio wachezaji pekee wakiwa hapa wataona na watakuwa mabalozi watakaporudi kwenye taifa lao, nao watashajiisha wengine kuja kutembelea Zanzibar,” amesema. 

“Huu ni mwelekeo mzuri mashindano kama haya kufanyika hapa Zanzibar kwa mara ya kwanza inaonesha namna gani tunavyozidi kuchanja mbuga kusonga mbele kimataifa."

Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni Utalii, Arif Abbas Manj amesema sekta ya utalii ndio inachangia asilimia kubwa ya uchumi wa Zanzibar na kwamba wamejipanga kuhakikisha wananchi wote wanaofika wanapata sehemu nzuri za kulala.

“Hii ndio dhana halisi ya utalii tumejipanga wananchi wajitokeze kwa wingi kushuhudia mechi hii.

 Zipo hoteli za kutosha wasihofu tunawakaribisha,” amesema