Masaa matano mazito Yanga

ACHANA na tukio la Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla kutolewa maneno machafu na mashabiki baada ya kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 na Kagera Sugar.

Mechi ilipoisha tu, vigogo wote unaowajua wa Yanga waliwasha magari yao na kulifuata nyuma basi la wachezaji mpaka kambini - Kigamboni, huku wachezaji wakijua kwamba ni ishu ya kawaida tu na yataisha goma likageuka.

Iko hivi; walipofika kambini tu wachezaji walipitiliza vyumbani kuoga na baadaye kula.

Lakini kwenye mida ya saa tano wakiwa wanajiandaa kwenda kulala mara paap! Akaibuka Meneja Hafidh Saleh na kutoa ujumbe kwa kapteni Lamine Moro kwamba wachezaji wote wanatakiwa kwenye ukumbi wa mikutano. Makocha wakaambiwa wasubiri kidogo nje.

Walipoingia ukumbini wakakutana na vigogo kibao wa Yanga wakiongozwa na Msolla, Hersi Said ambaye ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Usajili pamoja na Senzo Mazingisa ambaye ni mshauri wa Yanga kwenye mabadiliko. Baada ya Salamu wakaulizwa tatizo ni nini, mbona timu inayumba?

Wakiwa wanajiandaa kujibu wakasisitizwa kwamba wawe wawazi kwani kikao hicho kitakuwa ni siri kubwa baina yao na viongozi na kila kitu kitaishia ndani - hapo, lengo likiwa ni kujenga na kurudi kwenye ramani ya ushindi.

Wachezaji hao wakaanza kufunguka kwamba hata wao wanashindwa kuelewa ni nini kinatokea kwa vile hata wao hawapendi kuona hali hiyo.

Lakini sababu kubwa tatu walizowaeleza viongozi ni kwamba matokeo hayo yanatokana na mabadiliko ya kiufundi yanayofanywa na kocha mara kwa mara kikosini, uwepo wa majeraha ndani ya kikosi pamoja na nidhamu ya mchezo miongoni mwao.

Baada ya sababu hizo viongozi wakauliza kama kuna tatizo lolote ambalo linasababishwa na uongozi au malimbikizo yoyote wanayodai na wachezaji wakasema hakuna, ila lipo upande wao uwanjani.

Kikao hicho kikamalizika wakaruhusiwa kwenda kulala majira ya saa sita usiku ndipo likaitwa benchi la ufundi likiongozwa na Cedrick Kaze.

Walipoingia makocha wakaelezwa kile walichosema wachezaji, lakini uongozi ukawahakikishia kwamba uko upande wao kama wanavyofanya kwa wachezaji na watazidi kuwasapoti kwa kila hali, na wanaelewa kwamba ni changamoto za kazi.

Baadaye kila kocha akapewa nafasi ya kuzungumza, lakini Kaze akawaambia kwamba mbio za ubingwa bado kabisa na matokeo kama hayo kwenye ngwe ya pili siyo kitu cha ajabu.

Aliwaelezea pia kuwa lengo lake la kubadili kikosi na kuongeza ushindani linafanywa duniani kote na amekuwa akifanya tangu mwanzo na timu ilikuwa ikishinda.

Majadiliano hayo na makocha yalimalizika saa 10 alfajiri na kutoka na kauli moja kwamba kuanzia sasa ni ushindi kama kawaida na wala hakuna tatizo lolote ndani ya kikosi hicho wala sababu yoyote ya kupaniki.

HERSI AFUNGUKA

Kuhusu uwepo wa kikao hicho, Hersi licha ya kutotaka kuingia kiundani, alisema baada ya mazungumzo yao na timu nzima hivi sasa wanaamini mambo yatarejea haraka kwenye hali yake.

“Kuna mambo ambayo ni ya ndani kama klabu, lakini niseme kuna upepo mbaya ulikuwa unapita, tumezungumza na timu nzima, tumejua wapi kulikuwa na shida. Yote ya kuyafanyia kazi tumewaachia makocha kwa kuwa yako chini yao, mashabiki wetu niwaombe kwamba hata sisi viongozi tumeumia kwa matokeo haya lakini tunaamini sasa tunarudi tukiwa imara kuanzia mchezo wa Jumamosi,” alisema Hersi ambaye pia anaongoza Kamati ya Mashindano.

“Inawezekana yapo mengi ambayo ya kiufundi, ndio maana nasema tunawaachia makocha yale ambayo yanahitajika kufanyiwa kazi kama uongozi tutayafanyia kazi.

Aliongeza kuwa: “Ni kwamba hakuna shida ya kiutawala kwa maana ya wachezaji kukosa chochote wanachohitaji. Kama viongozi au wadhamini tumekuwa tukitimiza karibu kila kitu kwao, tuwaachie wao kwa kuwa wameahidi kurejea na nguvu kubwa.”

KAZE afunguka

Kocha Kaze amesisitiza kwamba bado hawajatoka katika mbio za ubingwa kwa kuwa wanaamini kwamba wanayo nafasi kubwa tofauti na watu wanavyodhani.

“Matokeo haya yametuhuzunisha wote, jambo zuri ni kufanyia kazi yale ambayo yametusababishia matokeo haya,” alisema Kaze ambaye ni raia wa Burundi. “Tutaanza na safu ya ulinzi, hili ndio eneo ambalo limetuangusha tumefanya makosa mengi yasiyo na ulazima, tuna kazi ya kufanya katika kurudisha utulivu katika ulinzi.”

Lamine aomba radhi

Akizungumzia matokeo waliyoyapata, nahodha wa Yanga, Lamine aliwaomba radhi mashabiki wao.

“Matokeo yanatusikitisha, tulipambana mwisho katika dakika za mwisho lakini hata hivyo hatukuwa na bahati,” alisema nahodha huyo.

“Nawaomba radhi (mashabiki) kwa matokeo haya, tunajua sote jinsi gani tumeumia, lakini tunatakiwa kuendelea tukiwa familia moja, nawaomba mashabiki wetu wapendwa kuendelea kuwa nasi Jumamosi, tunawaahidi tutarudisha nyuso za tabasamu, hatutakata tamaa.” Tangu mzunguko wa pia uanze, Yanga imepata sare tatu dhidi ya Prisons, Mbeya City na Kagera Sugar.