Kocha Simba ampa mchongo Kaze

SARE ya mabao 3-3 iliyopata Yanga juzi dhidi ya Kagera Sugar, imeongeza presha kwa msahabiki wa Yanga na kuanza kuwanyooshe vidole mabosi wao, lakini Kocha wa zamani wa Simba, Salum Madadi amekifichua kinachoitesa timu hiyo na kumpa mchongo Kocha Cedric Kaze.

Hiyo ilikuwa sare ya tatu mfululizo tangu duru la pili lianze ikianza na ile ya Tanzania Prisons na Mbeya City na kuzidi kutoa nafuu kwa watani wao walio na michezo miwili mkononi ya viporo wanaochuana nao kwenye kuwania ubingwa wa msimu huu.

Matokeo ya sare hizo mfululizo yametajwa na Kocha Madadi kuwa ni ya kawaida katika timu yoyote huku akitaja kwa klabu kama Yanga hata presha ya mashabiki na ile tamaa ya kutaka kuongoza muda wote kwenye msimamo na kutwaa ubingwa navyo ni chanzo cha matokeo hayo.

“Bado Yanga iko vizuri sana, timu inacheza kwa juhudi, inapambana na katika mpira sare ni matokeo ya kawaida na inaweza kupata timu ngumu au bora dhidi ya timu dhaifu au ya kawaida,” alisema Madadi aliyewahi pia kuinoa timu ya taifa na kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF.

“Kuna sababu nyingi za matokeo hayo, inaweza ikawa ni wingi wa mechi au namna wapinzani walivyowasoma na maandalizi, pia presha ya mashabiki au wachezaji wenyewe inaweza kusababisha perfomance kushuka,” alisema Madadi aliyesisitiza anazungumza kama mdau na sio kwa cheo chake. Alisema kama timu zote mbili ni bora, lazima mechi iwe ‘tafu’ na ubora wa timu haupaswi kuangaliwa kwa timu moja, hata namna wapinzani walivyojiandaa na saikolojia ya wachezaji wako ilikuwaje kabla ya mechi,” alisema.

Akiizuingumzia mechi ya juzi, Madadi alisema hakuona dalili za uchovu kwa timu zote mbili.

“Kipindi cha kwanza, Kagera Sugar ilicheza huru na kwa kujiamini hiyo pekee ilikuwa ‘advantage’ kwao. Yanga ndio ilikuwa na presha zaidi na Kagera haikuwa na cha kupoteza na mnapokutana na timu ambayo haina cha kupoteza huwa hamtulii kuanzia kwenye benchi na hata nje ya uwanja.”

Alisema bado Yanga haijapoteza dira ya ubingwa, kwani kwa mechi zilizosalia kabla ya msimu kuisha ni nyingi na gakuna timu yenye uhakika na ubingwa kwa sasa.

“Mechi 14 ni nyingi sana, kinachohitajika ni wachezaji hasa wale wenye sifa za kuwa viongozi uwanjani kuwasaidia wenzao kupunguza paniki na kuwatuliza wenzao ndani ya uwanja,” alisema Madadi na kuongeza;

“Presha ya mashabiki kuishusha ni timu kupata matokeo, hivyo kama wachezaji wata ‘relax’ na kucheza bila paniki, hakuna shaka watarudi kwenye mstari mzuri zaidi, japo hawako kwenye alama mbaya.”

Kingine ni benchi la ufundi kipindi hiki ambacho presha ni kubwa kuwa na jukumu la kuwaelekeza wachezaji kuliko kuwalaumu.