Mara paap! Julio huyoo fasta Mwadui

WAKATI ikionekana kama Kocha Amri Said ‘Stam’ anajiondoa kwenye timu ya Mwadui ya Shinyanga, tetesi za kutajwa kwa Kocha Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’ zinasikika.
Tetesi za Julio kutajwa kwamba anaweza kukabidhiwa timu hiyo endapo Stam na Mwadui hazitalandana, ziliongezeka zaidi kufuatia Julio kuwa uwanjani wakati timu hiyo ilipocheza hapa Dodoma wiki iliyopita.
Katika mchezo huo, Mwadui waliofungwa mabao 3-1 na JKT Tanzania, ndio ulioanzisha zaidi minong’ono wa uwezekano wa Julio kuwa mmoja ya watakaoiongoza timu hiyo kumalizia msimu wa ligi unaoelekea ukingoni.
Hata hivyo, Julio alipoulizwa na Mwanaspoti juu ya uwezekano wake kuinoa timu hiyo endapo mabosi wa timu hiyo watashindwana na Amri, alipinga kuhusu mpango huo akisisitiza bado ni kocha wa timu ya vijana.
‘‘Kuwepo pale uwanjani siku ile wala sio sababu ya kwamba ninajiandaa kuifundisha timu ya Mwadui, nipo Dodoma na siwezi kufanya uamuzi huo, mimi bado ni kocha wa timu ya taifa ya vijana, hakuna kitu kama hicho’’ alisema Julio.
Julio ambaye aliweka rekodi ya kuwa kuipeleka timu ya vijana wa miaka 20 ‘Ngorongoro heroes’ kwenye mashindano ya Afcon, ndiye aliipandisha ligi kuu timu ya Mwadui kabla ya baadaye kujiondoa kwa sababu binafsi.
Imeandikwa na MATEREKA JALILU