Manji, Rostam Aziz na GSM sasa basi!

Muktasari:

KUREJEA kwa Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji kumeibua picha jipya ndani ya klabu hiyo ambalo limewapa jeuri wanachama kutamka kwamba; “Sasa unyonge basi.”

KUREJEA kwa Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji kumeibua picha jipya ndani ya klabu hiyo ambalo limewapa jeuri wanachama kutamka kwamba; “Sasa unyonge basi.”

Ingawa bado hadi jana Manji alikuwa na changamoto zake na vyombo vya dola, lakini watu wa karibu na bilionea huyo ambao wengine ni vigogo wa Jangwani walithibitisha kwamba amewahakikishia anarejea klabuni.

Mmoja wa vigogo wa Yanga aliiambia Mwanaspoti jana kwamba Manji atakuwa miongoni mwa wawekezaji wanne kwa mujibu wa mfumo mpya wa mabadiliko ya kiuendeshaji ambao utaanza kutumika ndani ya Yanga miezi miezi michache ijayo kama ikiridhiwa na mamlaka husika ikiwemo wanachama.

Alidokeza kwamba matajiri wengine wawili ambao wataungana na Manji ni Ghalib Mohammed ‘GSM’ ambaye ndiye anayeibeba Yanga kwa sasa pamoja na mfanyabiashara, Rostam Aziz ambaye amekuwa akiwapiga tafu klabuni hapo kimyakimya bila ya kupiga makelele.

Katika mfumo mpya wa uwekezaji ulioko ndani ya mabadiliko yanayokuja Yanga ni kwamba asilimia 51 za hisa zitabaki kwa wanachama huku wawekezaji ambao wanapendelea wawe Ghalib, Manji na Rostam watagawana asilimia 49 zilizosalia.

Viongozi wa Yanga waliozungumza na Mwanaspoti jana wanaamini kwamba mabilionea hao watatu endapo watakubaliana na kuomba kugawana asilimia 49 hali ya Yanga itakuwa moto wa kuotea ndani na nje ya uwanja zaidi hata ya zilivyo Simba na Azam kwa sasa.

Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Matawi ya Yanga, Shaaban Hudah aliliambia Mwanaspoti kwamba Manji ni mwanachama mwenzao na kwamba hawana kinyongo naye na kurejea kwake ni furaha kubwa kwao.

Hudah alienda mbali zaidi akisema hata kuhudhuria Mkutano Mkuu wao utakaofanyika Juni 27 Jijini Dar es Salaam ni ruksa kwani ndio utaanza kuchakata ishu hiyo ya mabadiliko.

Ujio wa Manji ambaye alikuwa nje ya nchi kwa miaka kadhaa, unaweza kuleta sura mpya ya Yanga yenye ushindani endapo ataamua kurudisha nguvu yake katika sura mpya ya uwekezaji wa ndani ya klabu ambayo alijijengea jina miaka kadhaa iliyopita.


MANJI ATIKISA SIMBA

“Kama (Manji) atarudi au vinginevyo hayo ni mambo yao, ila wasijisahaulishe kuwa hata Manji alipokuwepo tuliwafunga, hivyo hiyo sisi haitusumbui,” alisema Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu.

“Waache sasa kutukimbia, kama wakitukimbia uwanjani Julai 3 basi tutawafuata pale pale klabuni kwao tukawafunge,” alitania Mangungu jana alipoulizwa ujio wa Manji kama atarejea upya Jangwani tangu alipojiuzulu Mei 22, 2017 baada ya kuwapa ubingwa wa tatu mfululizo wa Ligi na wa 27 kwao.

Katibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa amesema mkutano wa Juni 27 ni wa kihistoria na wanahitaji wanachama wengi zaidi washiriki.

“Kama Manji atakuja hatofukuzwa na hakuwahi kufukuzwa Yanga wala hakuna msimamo wa sekretarieti au uongozi wa juu, kuwa Manji akihitaji kurudi hatapewa fursa, hivyo milango ipo wazi kwake kurudi,” alisema Mfikirwa na kuongeza;

“Cha muhimu tu ni kukidhi vigezo, na mfumo wetu wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu unaruhusu wawekezaji zaidi ya mmoja, hivyo akitaka kurudi klabu haina neno, aje na si yeye tu, yeyote mwenye sifa za kuwekeza Yanga anaruhusiwa.”

Manji aliondoka Yanga miaka kadhaa iliyopita akiwa Mwenyekiti wa klabu, hali iliyofanya nafasi yake kukaimiwa kwa muda kabla ya Yanga kutangaza uchaguzi.

Waliokuwa viongozi walidai nafasi ya mwenyekiti haigombewi kwani Manji atarejea, hali iliyosababisha Yanga kuwa kwenye kipindi cha mpito uliopelekea kuendesha klabu kwa kuchangishana hadi walipofanya uchaguzi mkuu uliomuweka Mshindo Msolla madarakani na baadaye kupata ufadhili wa GSM.

Ingawa Mfikirwa amesisitiza kwamba kama wanachama wataridhia kwenye mkutano mkuu mabadiliko hayo, taratibu nyingine zitaendelea ili klabu kuanza kujiendesha kama kampuni.