Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maniche, Malale anga za kibabe

MANICHE Pict

Muktasari:

  • Maniche ameipandisha Mtibwa Sugar Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza kwake baada ya kushuka msimu uliopita, ikimaliza mabingwa wa Ligi ya Championship na pointi 71, akiungana na Mbeya City iliyomaliza ya pili kufuatia kukusanya pointi 68.

MAKOCHA, Awadh Juma ‘Maniche’ wa Mtibwa Sugar na Malale Hamsini wa Mbeya City, wameandika rekodi ya kuzipandisha daraja timu hizo kutoka Ligi ya Championship hadi Ligi Kuu Bara msimu ujao, huku wakiungana na wengine waliofanya hivyo pia.

Maniche ameipandisha Mtibwa Sugar Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza kwake baada ya kushuka msimu uliopita, ikimaliza mabingwa wa Ligi ya Championship na pointi 71, akiungana na Mbeya City iliyomaliza ya pili kufuatia kukusanya pointi 68.

Mbeya City inayonolewa na Malale Hamsini aliyerithi mikoba ya Salum Mayanga aliyetua Mashujaa FC, ameirejesha tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, huku kocha huyo akiweka rekodi ya kuipandisha timu kwa mara yake ya pili.

Kwa mara ya kwanza, kocha huyo aliipandisha JKT Tanzania msimu wa 2022-2023, baada ya kikosi hicho cha maafande kumaliza mabingwa na pointi 63, ikiungana na Kitayosce kwa sasa Tabora United iliyomaliza ya pili, kufuatia kufikisha pointi 60.

Licha ya ‘Maniche’ na Malale kuweka rekodi hizo msimu huu, ila wapo makocha wengine waliofanya vizuri kwa kuzipandisha timu kutoka Championship hadi Ligi Kuu Bara, jambo linalowafanya kuendelea kuimbwa kila uchwao, licha ya ugumu uliopo.

Aliyekuwa Kocha wa Tanzania Prisons, Mbwana Makata ana ufalme wake wa kuzipandisha timu kwenda Ligi Kuu Bara, baada ya kufanya hivyo na Alliance FC msimu wa 2018-2019, kisha Polisi Tanzania (2019-2020) na baadaye Dodoma Jiji (2020-2021).

Baada ya hapo, Makata akaweka rekodi nyingine ya kuipandisha Pamba Jiji FC Ligi Kuu msimu wa 2023-2024 na kuibua shangwe kwa wakazi wa Mwanza, baada ya kikosi hicho cha ‘TP Lindanda’ kusota kwa miaka 23, tangu kiliposhuka daraja mwaka 2001.

Kocha mwingine ni Joseph Lazaro aliyeipandisha Coastal Union anayoinoa kwa sasa msimu wa 2011-2012 na 2017-2018, kisha akiwa pia na Mgambo Shooting msimu wa 2012-2013 na baadaye akaipandisha African Sports zote za Tanga msimu wa 2015-2016.

Lazaro anayeifundisha Coastal Union baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Juma Mwambusi kuondoka, aliipandisha timu hiyo msimu wa 2011-2012, akiwa na Juma Kampila na wakati kikosi hicho kinapanda daraja msimu wa 2017-2018, alikuwa na Juma Mgunda.

Fredy Felix ‘Minziro’ anayeifundisha Pamba Jiji kwa sasa, aliipandisha Singida United (2017-2018), KMC FC (2018-2019), huku timu nyingine ni Geita Gold inayoshiriki Championship ikipambana kurejea tena aliyoipandisha msimu wa 2021-2022.

Kocha Hassan Banyai aliyefariki dunia Agosti 5, 2021, ameweka rekodi pia ya kuipandisha Moro United mwaka 2011, kisha Majimaji FC (2014-2015) na Njombe Mji FC (2017-2018), huku akichezea timu mbalimbali za Bandari FC ya Mtwara na Simba.

Makocha wengine ni Stephen Matata aliyeipandisha Transit Camp (2004-2005), Tanzania Prisons (2011-2012) na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022, huku Jumanne Challe akizipandisha timu za African Lyon (2015-2016) na KenGold msimu wa 2023-2024.

Meja Mstaafu, Abdul Mingange akaipandisha Mashujaa FC inayotesa kwa sasa Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-2023 kupitia mechi za mtoano ‘Play-Off’, ilipoishusha Mbeya City iliyorejea tena kwa msimu huu, baada ya kuifunga kwa jumla ya mabao 3-1.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma ‘Maniche’ alisema timu inapokuwa na uchumi imara na viongozi wazuri ni rahisi kupanda Ligi Kuu Bara, licha ya kukiri Championship ni ngumu na bila ya mikakati mizuri ni ngumu kutimiza malengo mliyojiwekea.