Manara amtaja Mo Dewji ishu yake Simba

ALIYEKUWA msemaji wa Simba Haji Manara amevunja ukimya na kueleza sababu zilizomtoa klabuni hapo na nafasi yake kupewa Ezekiel Kamwaga.

Haji Manara akizungumza na waandishi wa habari Dar, afunguka mengi

Manara ambaye alihudumu katika timu hiyo kwa zaidi ya miaka sita ameeleza sababu za kutolewa katika nafasi hiyo huku akitaja ni sababu za kibiashara na umaarufu.

Alisema kuwa licha ya kufanya kazi kwa miaka sita katika timu hiyo bila mkataba ila alijitolea vya kutosha kutokana na mapenzi yake kwenye klabu hiyo licha ya kudai kupewa tuhuma alizodai kuwa hazipo.

"Nakumbuka mwaka 2015, Simba ilikuwa ikipitia wakati mgumu sana lakini nilkiweza kujitolea kwa kuchangisha pesa kwa ajili ya kuwapa wachezaji wetu kupitia makundi mbalimbali  ya mitandano jamii ili kuendana na hadhi ya klabu lakini kwa sasa wameshindwa kuthamini mchango wangu" alisema.

Manara alisema kuwa kitendo cha kuondolewa ni kutokana na kile alichodai Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya timu hiyo Mohamed Dewji 'MO' alimtaka kuacha kutangaza bidhaa nyingine tofauti na zake, jambo alilodai alikataa kukubaliana nalo kwa alichodai kuwa alikuwa akifanya kazi Simba bila kuwa na mkataba wowote.

"Nimefanya kazi kwa muda mrefu bila ya mkataba, nikaamua kuingia mikataba mbalimbali na kampuni tofauti ajili ya kufanya matangazo jambo ambalo 'MO' lilimuudhi na kuamua kuniundia zengwe ili niondoke" alidai.