Manara amshukuru Aveva
ALIYEKUWA msemaji wa Simba Haji Manara amemshukuru aliyekuwa Rais wa timu hiyo, Evance Aveva kutokana na mchango mkubwa aliouonyesha kwa kumpa sapoti alipoanza kuhudumu katika timu hiyo aliyoitumia kwa zaidi ya miaka sita.
Manara ambaye alitenguliwa katika waadhifa huo amemshukuru Aveva kutokana na kumwamini na kuisaidia Simba kufika ilipo sasa.
"Namshukuru Aveva kwa kuwa alikuwa ni mtu muhimu sana kwangu, aliniamini na sikumuangusha kwani tulipambana katika mazingira magumu, lakini tulijua ipo siku Simba itasimama juu kama ilivyo kwa sasa baada ya kupitia changamoto kadha wa kadha," amesema Manara.
Pia anawashukuru viongozi wa Serikali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), waandishi wa habari na wadau mbalimbali wa soka nchini kutokana na mchango wao mkubwa uliomfikisha alipo.
"Bila Serikali, waandishi wa habari, TFF nisingekuwa hapa nilipo. Hivyo natoa shukuran zangu kwa kila mmoja na kuahidi kuendelea kushirikiana kwenye masuala ya soka," amesema.
IMEANDIKWA NA DAUDI ELIBAHATI