Simba yatwaa ubingwa, Azam wakimbia medali
Muktasari:
- Wakati Simba inakabidhiwa kombe lake, lakini tukio la kushangaza wachezaji wa Azam pamoja na kocha Florent Ibenge hawakwenda kuchukua medali zao za ushindi wa pili.
BAADA ya kusubiri kwa miaka minne hatimaye Simba imetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya kuichapa Azam kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba Zanzibar.
Wakati Simba inakabidhiwa kombe lake, lakini tukio la kushangaza wachezaji wa Azam pamoja na kocha Florent Ibenge hawakwenda kuchukua medali zao za ushindi wa pili.
Ubingwa huo unaifanya Simba kumaliza ukame wa kusubiri miaka minne tangu walipofanya hivyo mwaka 2021 na kupita kipindi cha ukame wa kuchukua makombe tofauti na ilivyofanya msimu huu chini ya kocha Steve Barker raia wa Afrika Kusini.
Hili ni Kombe la tano la Simba la CRDB, lakini likiwa ni la nne tangu liliporejea.
Hata hivyo, rekodi imeendelea kuwabeba Simba ambapo kila ilipofanikiwa kufika fainali kwenye michuano hiyo imefanikiwa kuchukua ubingwa huo.
MCHEZO ULIVYOKUWA
Kipindi cha kwanza timu zote zilicheza soka la tahadhari zikishambuliana kwa hesabu lakini Simba ndio ilimiliki mpira vizuri ingawa haikuwa na makeke mengi kwenye lango la Azam ambao walifanya kazi nzuri ya ulinzi.
Azam iliamua kuweka nguvu kubwa kwenye ulinzi ikiipa Simba wakati mgumu ikishindwa kufungua ukuta wa matajiri hao wa Chamazi hali ambayo iliufanya mchezo huo kumaliza dakika 45 za kwanza kwa shuti moja tu lililolenga lango.
BATO KITAMBAA, TOURE
Kulikuwa na vita moja kubwa ya kibabe kati ya beki wa Simba, Ismael Toure na mshambuliaji wa Azam, Japhte Kitambala ambao walikuwa wakipambana kuzuiana kwa nguvu na akili huku mara kwa mara vita yao ikiamuliwa na mwamuzi wa mchezo huo, Sifu Amon.
Ilikuwa kama Azam inashambuliwa kwa kona au mpira wa adhabu basi Kitambala mtu wake ni Toure wakionyeshana umwamba.
Simba ikiwa inashambuliwa vita hiyo inageuka, Kitambala anakuwa chini ya ulinzi wa beki huyo mpaka mshambuliaji huyo akapewa kadi ya njano dakika ya 16 tu kutokana na mvutano wao.
DAKIKA 45 HAKUNA SHUTI LA MAANA
Timu zote licha ya kujaribu kutengeneza mashambulizi lakini Simba ilifanikiwa kupiga shuti moja tu langoni mwa Azam ndani ya dakika 45 za kwanza.
Simba ilifanikiwa kupata bao dakika ya 62 kufuatia kiungo wa Azam Yahya Zayd kujifunga wakati akitaka kuokoa mpira wa adhabu ndogo iliyopigwa na na kiungo Eli Mpanzu na beki huyo wa Azam lijifunga wakati akiwa kwenye harakati za kuokoa.
KADI NYEKUNDU
Dakika ya 68, Azam ilipata pigo baada ya kiungo wake Feisal Salum 'Fei Toto' kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumpiga ngumi kiungo wa Simba Libasse Gueye.
Baada ya bao hilo Azam ikaonekana kupaniki kwa kuwa wachezaji wake kuanza kucheza kwa vurugu dhidi ya wenzao wa Simba.
Kocha Florent Ibenge dakika ya 74 akalazimika kumuita nahodha wake Lusajo Mwaikenda na kumtuliza kisha naye kuwakusanya wenzake na kuzungumza nao kisha wakaendelea kucheza kwa utulivu.
PAREDI LINAANZIA HAPA
Hata hivyo baada ya ubingwa huo, Simba kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Habari, Ahmed Ally ilitangaza kuwa leo itakuwa na paredi la ubingwa ukiwa ni siku moja tu baada ya Yanga kufanya paredi baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2025/2026.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Ahmed alisema kuwa paredi la ubingwa litaanzia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Buguruni, Ilala, Kigogo na kuelekea Jangwani sehemu ambayo ni makao makuu ya klabu ya Yanga.
"Napenda kuwatangazia kuwa kesho tutakuwa na paredi la ubingwa ambapo tutaanzia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere baada ya timu kutua baada ya hapo tutapita sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam, Buguruni, Ilala, Kigogo na tukifika pale Jangwani tutakuwa na kikao kidogo cha saa tatu au nne hivi," alisema Ahmed.