Makocha wa TFF waingizwa mkenge Dar

Nembo ya Shirikisho la Soka Tanzania
Muktasari:
Mchezaji huyo alikiri hilo jana, huku Kaimu Mkurugenzi wa TFF, Salum madadi akionekana kushangaa; “Tutachunguza tukijua anacheza Ligi Kuu, tutamuondoa haraka.” Jopo hilo limetangaza wachezaji 36 waliopatikana katika mchakato wa maboresho ya Taifa Stars ulioshirikisha mechi za mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
JOPO la wang’amuzi vipaji la Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) limeingizwa mkenge. Limetangaza wachezaji wapya 36 lakini likaingia mkenge kwa straika,Ramadhan Kapalamoto (Kinondoni) ambaye walidhania ni chipukizi wakamjumuisha kikosini kumbe ni mali ya Simba na alitemwa kwenye orodha ya Zdravko Logarusic na kupelekwa kwa mkopo African Lyon inayoshiriki Daraja la Kwanza.
Mchezaji huyo alikiri hilo jana, huku Kaimu Mkurugenzi wa TFF, Salum madadi akionekana kushangaa; “Tutachunguza tukijua anacheza Ligi Kuu, tutamuondoa haraka.” Jopo hilo limetangaza wachezaji 36 waliopatikana katika mchakato wa maboresho ya Taifa Stars ulioshirikisha mechi za mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Madadi alisema jopo hilo liling’amua vipaji 143 katika mchakato, lakini waliochukuliwa kwa sasa ni hao 36 tu.
Aliwataja waliochaguliwa ni makipa; Abdulaziz Khatib Haji (Mjini Magharibi), Abubakar Abbas Ibrahim (Tanga), Benedicto Mlekwa (Mara) na Mtindi Kheri Ali (Kaskazini Unguja). Mabeki wa pembeni ni Edward Mayunga (Kaskazini Pemba), Hussein Moshi (Tabora), Omari Kindamba (Temeke) na Shiraz Abdallah (Ilala).
Mabeki wa kati ni Abbas Ali Haji (Kaskazini Unguja), Ancy Abdon (Kagera), Emma Namwamba (Temeke), Hussein Akilimali (Njombe), Joram Nasson (Iringa), Kayombo Henrico (Ilala), Miraji Maka (Mwanza), Ramadhan Ame Ramadhan (Kusini Unguja) na Said Juma Ali (Mjini Magharibi).
Viungo ni Abubakar Mohamed Ally (Kusini Unguja), Hashim Magoma (Shinyanga), Juma Said Jega (Lindi), Mtenje Alban Juma (Tanga), Ryna Mgonyike (Temeke) na Yusuf Mpilipili (Temeke).
Washambuliaji ni Abdallah Kagumbwa (Temeke), Abrahman Othman Ally (Mjini Magharibi), Athanas Bayagala (Mbeya), Athanas Mdamu (Mwanza), Ayubu Hashim Lipati (Ilala), Chunga Said (Manyara), Mbwana Mussa (Tanga), Michael Mlekwa (Lindi), Mohamed Seif Said (Kusini Pemba), Omar Nyenje (Mtwara), Paul Bundala (Ilala), Ramadhan Kapalamoto (Kinondoni) na Roman Nyapunda (Temeke).
Madadi alisema wastani wa umri wa wachezaji hao ni miaka 21, watafanyiwa vipimo vya afya kesho Jumatano na Alhamisi kabla ya kuingia kambini Ijumaa, Tukuyu mkoani Mbeya.
Timu hiyo itakuwa chini ya Madadi akisaidiwa na makocha Hafidh Badru, Salum Mayanga na Patrick Mwangata.
Aprili 13 mwaka huu utafanyika mchujo ili kupata wachezaji wa mwisho watakaoungana na wa Taifa Stars watakaoingia kambini Aprili 22 mwaka huu.
Taifa Stars inacheza mechi ya kirafiki mapema mwezi Mei mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi za mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika (Afcon) zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.