MAKALA MAALUM ANGUKO LA TP MAZEMBE: Baada ya kuokoteza wachezaji, Katumbi ashindwa kuiokoa-5

KATIKA toleo lililopita tuliona jinsi rais wa TP Mazembe, Moise Katumbi alivyoikimnia nchi baada ya kuonesha nia ya kugombea urais wa DRC mwaka 2016.
Wakati wa utawala wa Laurent Kabila, Katumbi aliikimbia DRC na kwenda uhamishoni Zambia kufuatia harakati zake za kisiasa kumfanya aonekane kitisho kwa mamlaka.
Laurent Kabila alipofariki dunia na nafasi yake kuchukuliwa na mwanaye Joseph, hali ilitulia na Katumbi akarudi nyumbani. Sasa inaendelea

Katumbi hakuacha harakati zake za kisiasa lakini alikuwa upande wa Rais Joseph Kabila akiwa mwanachama mtiifu wa chama tawala cha PPRD ambacho mwenyekiti wake alikuwa Rais Kabila mwenyewe.
Mwaka 2007 aligombea kiti cha Gavana wa Katanga na kushinda kwa kishindo, akitumia tiketi ya chama cha Joseph Kabila.
Mwaka 2015 Katumbi alitofautiana na Rais Kabila kuhusu kuheshimu katiba ya nchi. Katiba ilikuwa inasema Rais anatakiwa kutawala kwa vipindi viwili vya kidemokrasia.
Lakini Rais Kabila alitaka kubadilisha katiba ili agombee tena kwenye uchaguzi uliokuwa unakuja, mwaka 2016.
Katumbi akamshawishi Rais asifanye hivyo kwa kuheshimu katiba lakini pia kwa heshima yake mwenyewe kama Rais.
Moyoni, Katumbi alitaka agombee yeye pale Kabila atakapokubali kuiheshimu katiba, lakini Kabila akagoma na akamuona Katumbi kama kitisho.
Hapo ndipo hali ikabadilika kwa Katumbi na ndipo Septemba 2015 akajiuzulu ugavana na kuikimbia DRC, na kwenda uhamishoni.
Huku nyuma Kabila akapigwa presha na jumuia za kimataifa na kukubali kuheshimu katiba...akafuta nia yake ya kugombea tena.
Katumbi akarudi akiamini sasa mambo yamekuwa sawia. Lakini Kabila alikuwa bado madarakani na aliendelea kumuona kitisho.
Akamfungulia kesi kadhaa, ikiwemo ya uhaini kwa tuhuma za kukodi mamluki kuipindua serikali.
Akatoroka tena safari hii akienda uhamishoni Ubelgiji. Huku nyuma kesi ikasikilizwa na kukutwa na hatia. Akahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela bila  mwenyewe kuwepo.
Wakati mgogoro unaanza mwaka 2015, TP Mazembe walishinda ubingwa wa Afrika, ambao ulikuwa wa tano kwao na wa tatu chini ya uongozi wa Katumbi.
Lakini Katumbi alipoikimbia nchi na kuwaacha Mazembe kama mabingwa watetezi walipata mshtuko ambao uliwatingisha na kujikuta wakivuliwa ubingwa na Wydad Casablanca, kwenye raundi ya pili ya mashindano.
Kimsingi timu ikitolewa kwenye raundi ya pili huangukia Kombe la Shrikisho, na ndivyo ilivyokuwa kwa TZ Mazembe...wakajipanga vizuri na kushinda ubingwa.
Lakini mtikisiko wa kuondoka kwa Katumbi uliwatingisha hadi kwenye misingi ya klabu yao.
Japo ubingwa wa ligi ya ndani waliendelea kuushinda hadi sasa, lakini kwa Afrika hawakuwa tena na nguvu zile 2007 hadi 2015.
TZ Mazembe ikatoka kuwa klabu ya kusajili wachezaji nyota wa bei mbaya na kuwa klabu ya kuokoteza masalia ya klabu nyingine.
Kwa mfano, mwaka 2019 ilimsajili Ramadhan Singano ambaye aliachwa na Azam FC. Mwaka 2020 ikamsajili Eliud Ambokile zao la Mbeya City ambalo lilishindwa kucheza Afrika Kusini kwenye klabu ya Black Leopards.
TP Mazembe ikageuka kuwa klabu ya kubahatisha wachezaji kiasi kukusanya kundi la wachezaji zaidi ya 40 kambini kwao iliowapata kwa kuokotaokota. Inawakusanya na kuwaweka kambini halafu kocha anapewa uhuru wa kuwaangalia kuona nani anayemfaa amuingize kwenye vitabu vya klabu.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa kina Singano na Ambokile kutoka Tanzania na wengine wengi kutoka kila sehemu Afrika. Wachezaji  hawa waliweza kukaa tu klabuni hadi miaka mitatu bila kusajiliwa japo wana mikataba na klabu. Kusajiliwa maana yake kuhahalisha uwepo wa mchezaji ili aweze kucheza mechi rasmi.


KWANINI TP MAZEMBE ILIFIKIA HUKO?
Ni kwa sababu waliamini kwamba katika okota okota yao ya wachezaji wanaweza kubahatisha wawili watatu wenye uwezo wa kuibeba klabu. TP Mazembe haikuwa tena na bajeti ya kufuru tangu Katumbi aache ugavana 2015.
Katumbi akiwa gavana alitumia pesa nyingi sana za serikali kuwekeza kwenye timu.
Licha ya misukosuko ya kuikimbia nchi Mei 2016, Katumbi alirejea DRC Aprili 2019 baada ya uchaguzi kufanyika Desemba 2018 na Rais Felix Tshisekedi kupatikana.
Tangu 2019 pale Katumbi aliporudi nyumbani kutoka uhamishoni ingewezekana kabisa  kwa sasa TP Mazembe kurudi kwenye ubora wake, lakini imeshindikana kwa sababu mrija wa pesa haupo tena. Katumbi ni mfanyabiashara tajiri sana, lakini hawezi kuwekeza kiasi kikubwa cha pesa kutoka mfukoni mwake kama alivyofanya wakati akiwa gavana.
Kutokana na kupungua bajeti, TP Mazembe imekosa nguvu ya kushindana na klabu zenye bajeti kubwa kutoka sehemu nyingine ya Afrika na ndiyo maana inakwama kimataifa kwa sasa.
Tangu wawe mabingwa wa Afrika 2015, mafanikio pekee makubwa ni nusu fainali ya 2018/19. Hii siyo TP Mazembe ya Gavana Katumbi. Ni TP Mazembe ya mfanyabiashara Katumbi. Ile ya gavana kuanzia 2007 hadi 2015 isingepoa namna hii.


HITIMISHO
Katumbi ameshatangaza nia ya kugombea urais kwenye uchaguzi ujao wa DRC, Disemba mwaka huu, kushindana na Rais wa sasa Felix Tshisekedi.
Katika uchaguzi uliopita, licha ya yeye kuzuiwa kugombea, alimuunga mkono mgombea wa upinzani, Martin Fayulu, ambaye wengi waliamini alistahili kushinda kama siyo udanganyifu wa kura.
Endapo atashinda, kuna uwezekano mkubwa sana TP Mazembe ikarudi ilikokuwa, yaani kwenye kilele cha ushindani wa kweli kwenye soka la Afrika.