MAKALA MAALUM: Anguko la TP Mazembe -3

KATIKA sehemu iliyopita tuliona ni namna gani siasa za nchi, kukosa udhamini na siasa za ndani za klabu ziliposababisha anguko la kwanza la TP Mazembe.

Katika toleo la leo, tutaona namna ujio wa Moise Katumbi Chapwe ulivyoiinua klabu hiyo na kutawala tena, siyo tu Congo bali Afrika.


Sasa endelea...

 Chini ya utawala wa Raphael Katebe Katoto, hali ya kisiasa ndani ya klabu ilitulia.

Raphael Katebe Katoto, mfanyabiashara tajiri wa Lubumbashi na mwanasiasa wa chama cha upinzani cha RCD Goma, aliachia ngazi klabuni kwa hiyari yake ili aelekeze nguvu kwenye siasa, mwaka 1997.

Itakumbukwa kwamba mwaka huo ndiyo Laurent Desire Kabila aliingia madarakani kwa kumpindua Mobutu Sese Seseko.

Mojawapo ya mambo aliyoyabadilisha ni pamoja na jina la nchi, kutoka Zaire hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katika kuiishi Demokrasia, Kabila aliruhusu vyama vya siasa kufanya kazi kwa uhuru, na ndipo Raphael Katebe Katoto alipotaka kuutumia uhuru huo kujiimarisha kisiasa.

Nafasi yake kama Rais wa TP Mazembe akamuachia mdogo wake anayechangia mama, Moise Katumbi Chapwe.

Moise Katumbi akiwa na miaka 33, aliichukua TP Mazembe akiwa na lengo la kuendeleza utulivu wa kisiasa ndani ya klabu kama alivyofanya kaka yake, lakini kuiimarisha kiufundi na kitaasisi ili kuirudisha klabu hiyo kwenye hadi inayostahili.

Katumbi alikuwa mfanyabiashara mdogo mwenye pesa nyingi na mhemko mkubwa wa soka ukichagizwa na mapenzi yake makubwa kwa klabu ya nyumbani ya TP Mazembe.

Moïse Katumbi alizaliwa Desemba 28, 1964 kutoka kwa mama mwenye asili ya Congo na baba Mgiriki mwenye asili ya Uyahudi.

Baba yake mzazi anatokea kisiwa cha Rhodes cha Ugiriki na alikimbia kisiwa hicho mwaka 1938, baada ya serikali ya kifashisti ya Italia kuweka sheria kali za kibaguzi.

Italia ilikikalia kimabavu kisiwa hicho tangu mwaka 1912. Kwa hiyo alipokimbilia Kongo, wakati huo ikiwa chini ya ukoloni wa Ubelgiji, akaloewa Katanga kwenye mjini wa Elisabethville, ambao sasa ndiyo Lubumbashi.

Akiwa hapo akakutana na mwanamke mzawa na kuzaa naye mtoto ambaye ndiyo huyo Moise. Lakini mtoto huyo akachagua kutumia jina la ubini wa upande wa mama yake, badala ya upande wa baba yake.

Na sababu ni agizo la Rais Mobutu SeseSeko mwaka 1971 kuacha kutumia majina ya kigeni na kutumia majina yenye asili ya nyumbani.

Nchi hiyo ilikuwa ikiitwa Congo - Leopoldville, kuanzia mwaka huo ikaitwa Zaire. Leopoldville ndiyo ulikuwa mji mkuu, lakini kuanzia mwaka huo ukaitwa Kinshasa. Elisabethville ukaitwa Lubumbashi. Stanleyville ukaitwa Kisangani, na kadhalika.

Hata wanamuziki wakubwa wa Congo walibadili majina, Joseph Kabasele akajiita Pepe Kale, Franco akajiita Rwambo Rwanzo Makiadi, nk.

Kwa hiyo mtoto Moise naye akaacha kutumia jina la kizungu la baba yake la Nissim Soriano, na kutumia jina la asili ya Congo, la Katumbi...akawa Moise Katumbi.

Katumbi aliipata elimu yake hapo hapo Lubumbashi na kuanza biashara zake hadi kufikia kuwa tajiri mkubwa.

Alikulia kwenye kijiji cha Kashobwe karibu na ziwa Mweru, mpakani na Zambia.

Baba yake mzazi alijihusisha na biashara ya uvuvi na samaki kwenye ziwa hilo, na ndipo Katumbi mwenyewe alipoanzia biashara zake.

Akiwa na miaka 13, alianza biashara ya kuuza samaki wa maji chumvi na maji baridi kwa kampuni kubwa ya serikali ya uchumbaji madini ya Gecamines.

Biashara ya samaki ikamfungulia mlango kupitia kampuni hiyo ya madini na kilichofuata baada ya hapo ni kuzaliwa kwa bilionea mkubwa sana.

Akafungua makampuni yake na kuzidi kujiimarisha kiuchumi na hadi kufika mwaka 1997 alipoichukua TP Mazembe, alishakuwa tajiri mkubwa sana.

Mwaka huo 1997, Moise Katumbi alianzisha kampuni ya madini ya MCK (Mining Company Katanga) na moja kwa moja akaifanya kampuni hiyo kuwa wadhamini wa TP Mazembe.

Hapo ndipo klabu hiyo ilipoanza kuamka tena na kuanza kujiimarisha kuanzia soka la ndani.

Mwaka huo, 1997, kwa mara ya kwanza TP Mazembe wakafika nusu fainali ya ligi kuu tangu 1988.

Ligi ya Congo huchezwa kuanzia ngazi ya majimbo halafu kuna timu zinafuzu kwa ajili ya ligi ya kitaifa, kutegemea na mwaka husika. Kwa mwaka 1997, timu tatu kutoka kila jimbo zilifuzu.

TP mazembe kutoka jimbo la Katanga ilifuzu hadi nusu fainali na kutolewa na AS Vita kwa kipigo cha 3-0.

Lakini hii ilikuwa hatua kubwa sana kwa timu ambayo kwa miaka 10 iliyopita mafanikio yao yalikuwa kuvuka hatua ya majimbo tu halafu kwenye ligi ya kitaifa inatolewa raundi ya kwanza.

Kidogo kidogo TP Mazembe ikazidi kuimarika na kuonesha matumaini ya kurudi inakostahili.

Wakati mambo yakianza kunoga, machafuko ya kisiasa yakatokea nchini humo na Rais Laurent Desire Kabila akaanza kuwaandama watu anaowaona tishio.

Moja ya watu hao ni Moise Katumbi, ambaye kaka yake alikuwa mwanasiasa kama tulivyoona kule juu, na yeye mwenyewe alishaanza kuonesha shauku ya kisisiasa.

Mwaka 1999, Katumbi akaikimbia nchi na kwenda uhamishoni Zambia kutafuta hifadhi ya kisiasa.

Lilikuwa pigo kwa TP Mazembe kwani matumaini waliyoanza kuyaona ghafla yakaanza kufifia.


Itaendelea.....