MAKALA MAALUM ANGUKO LA TP MAZEMBE: Mihela yamwagwa kwa mastaa -4

Katika toleo lililopita tuliona jinsi hali ilivyoanza kubadilika ndani ya klabu ya TP Mazembe lakini ghafla siasa za nchi zikaharibu mambo.
Katika toleo hili tutaona kilichofuata baada ya pale. Endelea...

Mwaka 2001 Rais Laurent Desire Kabila aliuawa na nafasi yake kuchukuliwa na mwanaye, Joseph Kabila. Ili kuijenga upya nchi, Joseph Kabila akawaomba kurudi nyumbani watu wote waliokimbia nchi hiyo kisiasa.

Katumbi akakubali lakini akachagua kurudi Julai 11, 2003 kuienzi tarehe ambayo Jimbo la Katanga lilijitangazia uhuru mwaka 1960. Julai 11 ni siku muhimu sana kwa watu wa Jimbo la Katanga na huienzi kila mwaka kama alama ya utaifa wao.

Kabila alimwomba Katumbi arudi kusaidia kuimarisha sekta ya madini na Katumbi aliporejea akaweka nguvu kwelikweli kwenye madini. Lakini hata hivyo, ule uwekezaji alioufanya ndani ya TP Mazembe tangu awe Rais wa klabu mwaka 1997 na kuanza kuleta matunda kidogo kidogo, ulifikia kilele mwaka 2000 na 2001 waliposhinda ubingwa wa ligi kuu mara mbili mfululizo wakati Katumbi akiwa Zambia.

Urejeo wake ukaja na awamu ya pili ya uwezekaji iliyoanza mwaka 2004. Hiki ndicho kipindi ambacho wachezaji kama kipa Robert Kidiaba na nyota kama Jean Kasusula walisajiliwa. Pia alisajiliwa Mtanzania Ngawina Ramadhan Ngawina ambaye sasa ni kocha wa timu ya ligi ya Championship, KenGold ya Chunya, Mbeya.

Ngawina alikuwa akiichezea klabu ya Bukavu baada ya kutoka Rwanda alikokuwa akiitumikia klabu ya Mukura Victory. Akaenda kufanya majaribio TP Mazembe na kufanikiwa, huku Dieumerci Mbokani aliyefanya naye majaribio akifeli na kuachwa.

Mihayo Kazembe ambaye hivi karibuni alikuwa kocha wa klabu hiyo, wakati ule alikuwa nahodha. Katumbi akawekeza kidogo kidogo na hatimaye uwekezaji wake ukairejesha TP Mazembe kwenye ubora wake.

TP Mazembe ikatawala ligi ya Kongo na kushinda ubingwa mwaka 2006, 2007, 2009, 2011, 2012, 2013, 2013/14 na 2015/16. Pia ikatawala Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda ubingwa mara mbili mfululizo; 2009 na 2010...halafu ikashinda tena mwaka 2015.

Mwaka 2010 pia ikafika fainali ya klabu bingwa ya dunia na kuweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Afrika kufanya hivyo. Wakati inashinda ubingwa wa Afrika mara mbili mfululizo mwaka 1967 na 1968, iliweka rekodi kwa kuwa klabu ya kwanza kufanya hivyo.

Rekodi hiyo ilidumu hadi ilipokuja kuvunjwa na Enyimba ya Nigeria ilipofanya hivyo mwaka 2003 na 2004. Na walipochukua tena mara mbili mfululizo 2009 na 2010, TP Mazembe ikaweka rekodi nyingine ya kuwa klabu ya kwanza kutwaa ubingwa mfululizo katika vipindi viwili.

Mwaka 2007, Katumbi alirudi kwenye siasa na kugombea ugavana wa Jimbo la Katanga. Akashinda kwa kura za Tsunami na kuwa "Rais wa Jimbo". Gavana ni mtu mkubwa sana kwa katiba ya nchi yao. Ana mamlaka ya kuelekeza bajeti ya jimbo katika miradi anayoona yeye inafaa.

Katumbi kama mfanyabiashara wa madini tangu zamani, aliisimamia serikali ya Jimbo la Katanga kuhakikisha inafaidika na madini yaliyopo jimboni humo. Zaidi ya kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo, Katumbi pia alitumia fedha za serikali kuwekeza TP Mazembe.

Ndipo walipojenga uwanja wao wa Stade de TP Mazembe uliozinduliwa mwaka 2011. Uwanja huu uliopo eneo la Kalamondo, ni wa kwanza Afrika kuwa na nyasi bandia za kisasa za kizazi cha tatu, wakati zinatoka tu. Akademi ya TP Mazembe ilikuwa na watoto zaidi 2000 wakilelewa na klabu.

TP Mazembe ikanunua ndege mbili binafsi na kuifanya kuwa klabu pekee ya Afrika kuwa na ndege zake binafsi mbili. Ndege ya kwanza ilikuwa Dornier 128 iliyotengenezwa Ujerumani ambayo ilinunuliwa mwaka 2009. Halafu mwaka 2011 ikaja ndege nyingine aina ya McDonnell Douglas MD-80 yenye uwezo wa kuchukua watu 140 na chumba maalumu cha VIP chenye vipi 16 tu.

TP Mazembe ilitisha kweli kweli. Katumbi aliamua kuwekeza kwenye klabu kwa kuweka mazingira mazuri kwa wachezaji kufanya kazi kwa maana ya miundombinu, pamoja na masilahi. Ngawina anasema mwaka 2004 aliposajiliwa TP Mazembe, Katumbi alikuwa anatoa Dola 500 kwa kila mchezaji kila wikiendi.

Kwenye makala ya War, Diamonds and Football ya CNN iliyoandikwa na mwandishi James Montague mwaka 2010 kuekelea fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia kati ya TP Mazembe na Inter Milan, mwandishi alimhoji mhariri wa habari za nje wa jarida la Monocle Magazine na mtunzi wa kitabu cha Africa United: How Football Explains Africa, Steve Bloomfield kuhusu uwekezaji wa Katumbi ndani ya klabu hiyo.

Steve Bloomfield akasema: "Nilikutana na Katumbi mjini Harare (Zimbabwe) wakati TP Mazembe ilipokwenda kucheza na mabingwa wa Zimbabwe kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Bajeti ya klabu ya Zimbabwe kwa mwaka ilikuwa Dola 200,000.

Lakini niliongea na Katumbi akasema wakishinda mechi hiyo kila mchezaji na makocha watapewa Dola 250,000. Yaani motisha ya TP Mazembe kwa mechi moja ilikuwa kubwa kuliko bajeti ya mwaka ya mabingwa wa Zimbabwe."

Kupitia maelezo haya unaweza kuona ni kiasi gani Katumbi aliwekeza kwenye klabu hiyo. Katumbi alikuwa anawalipa wachezaji wake nyota pesa nyingi ili kuwasahaulisha habari za kwenda kucheza Ulaya. Mwaka 2010 wachezaji wa TP Mazembe walikuwa wanalipwa Dola 3000 kwa wiki, katika nchi ambayo kima cha chini cha mshahara wa serikali ulikuwa Dola 120 kwa mwezi...pata picha!

Kwa mfano nyota wake Tressor Mputu Mabi alitakiwa na Arsenal, lakini aliamua kubaki TP Mazembe. Mwaka 2011 TP Mazembe walikuja Tanzania kucheza na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Wakamwona Mbwana Samatta na kumnunua kwa Sh150 milioni. Hizi zilikuwa pesa nyingi zilizowapagawisha Simba wakati huo. Hadi sasa Tanzania ni wachezaji wachache sana ambao usajili wao unafikia thamani hiyo.

Lakini kwa TP Mazembe, Samatta alikuwa mmoja wa wachezaji walionunuliwa kwa pesa kidogo sana. Wakati klabu ikiwa kwenye kilele cha neema na raha, Katumbi akaachia nafasi ya ugavana mwaka 2015 akiwa na nia ya kugombea urais wa nchi kwenye uchaguzi mkuu wa 2016. Hapo ndipo mambo yalipobadilika.

Rais aliyekuwepo madarakani, Joseph Kabila akamwona Katumbi kama kitisho kwake. Kesi za kisiasa zikaanza kumwandama na hatimaye mwezi Mei, mwaka huo akakimbilia uhamishoni Afrika Kusini. Kupoteza ugavana na kuwa nje ya nchi kukasababisha mwanzo wa anguko la sasa la TP Mazembe.
Itaendelea....