MAKALA MAALUM: Anguko la TP Mazembe - 2

Katika toleo lililopita, tuliona historia ya klabu ya TP Mazembe kuanzia mwanzo wake, maana ya jina lake na mafanikio yake ya miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Leo tutaangalia anguko la kwanza la klabu hiyo kuanzia katikati ya miaka ya 1970 hadi miaka ya mwanzoni mwa 2000, licha ya mafanikio madogo ya mwanzoni mwa miaka ya 1980.


Sasa endelea!
Société du Pneu Englebert au Englebert tyre company, yaani kampuni ya matairi ya Englebert, ilikuwa kampuni kubwa kutoka Ubelgiji, iliyoanzishwa mwaka 1898 na mtu mmoja wa kuitwa Oscar Englebert.
Kampuni hiyo ilikuwa kwenye harakati za kujitanua kibiashara na kuvuka mipaka ya nchi na bara lake kwa kutangaza bidhaa zake nje ya Ubelgiji na Ulaya kwa ujumla.
Ikafika Congo na kuinunua klabu hiyo katika wakati ambao nchi ya Congo ilitoka tu kupata uhuru na ilikuwa ikijitibu majeraha yake kutokana na machafuko yaliyosababisha kuuawa kwa waziri mkuu wa kwanza wa nchi hiyo, Patrice Lumumba.
Hata hivyo, licha ya kampuni hiyo kujaribu kuwekeza nje ya Ubelgiji na Ulaya, kule ilikotoka yaani Ubelgiji haikuwa ikifanya vizuri sana kibiashara.
Kuyumba kwa biashara yao kukasababisha kampuni hiyo itafute mbia na ndipo ilipoungana na kampuni nyingine ya matairi ya Uniroyal kutoka Marekani.
Uniroyal ilikuwa kampuni iliyotawala biashara ya matairi nchini Marekani na ilitaka kutawala Ulaya pia. Kwa hiyo ikafungua tawi lake barani humo.
Tawi hilo ndilo lililoungana na Englebert na muungano wao ukaleta kampuni mpya ya pamoja iliyoitwa Uniroyal Englebert ambayo ilirithi biashara za kampuni zile mbili huku kila kampuni ikibaki na baadhi ya hisa zake.
Lakini mwaka 1979, kampuni ya Uniroyal ikajitoa kwenye ubia na Englebert kuamua kuuza hisa zake zote za Ulaya kwa kampuni ya Continental Tyres.
Kufa kwa ubia wa Uniroyal kukaifanya kampuni ya Englebert kukosa pa kujishikiza, ikafa kifo cha asili na huo ndiyo ukawa mwisho wa Kampuni ya Englebert.
Kufa kwa kampuni hii kukasababisha anguko kubwa la kwanza la TP Mazembe liloanzia nusu ya pili ya miaka ya 1970 na kudumu miaka yote ya 1980 hadi miaka 1990.
Tangu wachukue ubingwa wa ligi kuu mwaka 1976, hawakuchukua tena hadi 1987, na baada ya hapo hawakuchukua tena mwaka 2000.
Maajabu pekee yalitokea mwaka 1980 walipojitahidi na kushinda kombe la washindi barani Afrika, ambalo lilikuwa likishirikisha washindi wa Kombe la FA la kila nchi.
Huo ulikuwa mwaka mmoja baada ya kampuni ya Englebert kufa, na kwa kiasi kikubwa TP Mazembe walikuwa bado na masalia ya uwekezaji wa kampuni hiyo
Lakini baada ya hapo jahazi likazama. Kukosa mdhamini wa uhakika na machafuko ya kisiasa katika jimbo la Katanga, hasa kwenye mji wa Lubumbashi ambako timu hiyo inatoka, vikaongeza matatizo.
Kiasili, jimbo la Katanga na mji mkuu wake wa Lubumbashi vimekuwa na ulegevu wa kisiasa kwa miaka mingi, tangu uhuru wa nchi hiyo.
Mwaka 1960, waasi wa Maimai Bakata Katanga walijitangazia uhuru na kupeperusha bendera yao ya Inchi ya Katanga kama walivyojiita wenyewe, chini ya kiongozi wao Moise Tshombe na chama chake cha CONAKAT.
Nchi ya Katanga au Jamhuri ya Katanga ilidumu hadi mwaka 1963 ilipoanguka baada ya uvamizi wa majeshi ya Umoja wa Mataifa na Katanga kurudi kama jimbo la Congo.
Machafuko haya yalikuwa makubwa kiasi cha kusababisha ligi ya Congo isifanyike katika miaka hiyo mitatu.
Tangu wakati huo hadi sasa Katanga haijawahi kuwa na utulivu kwa asilimia mia moja na ile roho ya kujitenga na Congo bado ipo.
Lubumbashi ni mji wa pili kwa ukubwa nchini DRC baada ya Kinshasa na kutokana na utitiri wa madini kwenye Jimbo la Katanga, mji huo umekuwa muhimu sana kiuchumi.
Lakini kwa sababu ya ulegevu wa kisiasa, matokeo yake madini hayawanufaishi vya kutosha raia wake ambao ndiyo mhimili mkuu wa klabu ya TP Mazembe.
Kuyumba kwa uchumi wa wananchi ndiyo kuyumba kwa uchumi wa mhimili wa klabu na ndiyo kuyumba kwa klabu.
Hayo yakawa yakiitafuna TP Mazembe na kuzidi kuididimiza klabu hiyo.
Katika miaka yote hii, TP Mazembe ilikuwa kwenye kivuli cha timu kubwa za Kinshasa, AS Vita, DC Motema Pembe CS Imana, AS Bilima na mbaya zaidi wapinzani wao wa Mji wa Lubumbashi,  FC Lupopo.
Ukiacha mambo ya kutoka nje ya klabu, siasa za ndani nazo zilikuwa tatizo kwa klabu hiyo.
Kutoka mwaka 1970 hadi 1975, klabu hiyo ilishuhudia viongozi watano wakija na kupinduliwa.
Wakati kampuni ya Englebert inakufa mwaka 1979, Rais wa klabu alikuwa Raphaël Katebe Katoto ambaye alidumu hadi 1981.
Machafuko ya kisiasa ndani ya klabu yakarudi na kusababisha mapinduzi yaliyomuangusha Katebe Katoto.
Klabu ikawa chini ya utawala wa mpito wa Tshilombo Mwen Tshitol kuanzia mwaka 1982 hadi 1983 alipokuja Somville.
Soville alijitahidi kutuliza hali ya kisisa ndani ya klabu na kudumu madarakani hadi mwaka 1997 alipoingia Moise Katumbi Chapwe, aliyepo hadi sasa.
Katika toleo lijalo tutaangalia ujio wa Katumbi na kuzaliwa upya kwa klabu hiyo.

Usikose kesho....