MAKALA MAALUM: Anguko la TP Mazembe -1

MWAKA 2010, klabu ya TP Mazembe kutoka Lubumbashi, DRC, ililiwakilisha vyema Bara la Afrika na kufika fainali ya klabu bingwa ya dunia.

Wapinzani wao kwenye mchezo wa fainali walikuwa Inter Milan ya Italia, ambao waliliwakilisha Bara la Ulaya.

TP Mazembe walishiriki klabu bingwa ya dunia kama mabingwa wa Afrika, na Inter Milan walikuwa mabingwa wa Ulaya.

Mwaka 2023, miaka 13 baadaye, Inter Milan wako fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya, wakiutafuta tena ubingwa huku TP Mazembe wakiwa hali mbaya, wakishindwa angalau kuvuka hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho.

Kwa msimu wa pili mfululizo, TP Mazembe wameshindwa kuingia hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa, wakitolewa na kuangukia Kombe la Shrikisho.

Mara ya mwisho kufika makundi ya ligi ya mabingwa ilikuwa msimu wa 2020/21, wakamliza wa tatu kwenye kundi.

Kwa miaka ya hivi karibuni, ufalme wa TP Mazembe uliokuwa kwenye ligi ya mabingwa, ulihamia kwenye Kombe la Shirikisho...lakini sasa na huko haupo tena.

Mara ya mwisho kushinda ligi ya mabingwa ilikuwa 2015. Misimu miwili uliyofuata, 2016 na 2017, walishinda mfululizo ubingwa wa kombe la shirikisho.

Baada ya hapo, imekuwa aibu sana kwao...hawaishi maisha yao kabisa.


Nini kimeikumba TP Mazembe?

Kupitia ukurasa huu, tutakuletea mfululizo wa makala za anguko la miamba hao wa Afrika.

Lakini kwa leo, hebu ifahamu kwanza kiundani klabu hii kigogo kabisa wa Afrika.


WATOTO WA BABA PAROKO

TP Mazembe ilianzishwa mwaka 1939 na watawa wa wabenedikti wa kanisa katoliki la Lubumbashi, ikiitwa Saint Georges FC. Mwaka 1944 ikabadili jina na kuwa Saint Paul F.C.


KUNGURU

Baada ya miaka kadhaa, timu ikatoka mikononi mwa kanisa na kurudi kwa wananchi na ikanunuliwa na kampuni ya matairi ya Englebert, na ndipo ikabadili jina na kuwa Englebert FC.

Licha ya kuwepo kwa mamba kwenye nembo yao, jina la utani la klabu hii ni KUNGURU, ambalo kwa lugha ya kilingala ni MAZEMBE. Na hii ni kutokana na rangi za jezi zao.


NGUVU KUPITA KAWAIDA

Mwaka 1966, klabu hii ikashinda ubingwa wa kwanza wa ligi ya Kongo, tena bila kupoteza hata mechi moja. Kutokana na hilo, wakajibatiza jina la T.P yaani Tout Puissant ikiwa na maana ya 'WENYE NGUVU KUPITA KAWAIDA". Ubingwa wa ligi ya Kongo ukawapa tiketi ya kushiriki Klabu Bingwa Afrika 1967, na kushinda ubingwa.


UBINGWA WA MEZANI

Ubingwa wa Afrika walioshinda 1967 waliupatia mezani baada ya wapinzani wao, Asante Kotoko ya Ghana, kutotokea uwanjani katika mchezo wa tatu wa fainali.

Timu hizo zilitoshana nguvu katika michezo miwili ya kwanza; wakianza kwa sare ya 1-1 mjini Accra na 2-2 Lubumbashi. Hakukuwa na sheria ya bao la ugenini wakati huo, wala mikwaju ya penati.

Na bahati mbaya hakukuwa na kanuni rasmi inayotoa mwongozo wa nini kifanyike katika mazingira kama hayo.

Refa wa mchezo akataka kurusha shilingi ili kumpata bingwa lakini katibu mkuu wa CAF akatokea na kusema utafanyika mchezo wa tatu katika uwanja huru. Vilabu vitapewa taarifa kupitia vyama vya soka vya nchi zao.

Mchezo huo ukapangwa kufanyika Yaounde Cameroon lakini Kotoko hawakutokea uwanjani. Kumbe CAF walipeleka taarifa kwa chama cha soka cha Ghana, lakini chama kikasahau kuiambia Kotoko...Mazembe wakapewa ubingwa wa mezani


UBINGWA WA REKODI

Mwaka 1968 wakatetea ubingwa wa Afrika na kuwa klabu ya kwanza kufanya hivyo. Miaka miiwili iliyofuata wakafika fainali, 1979 na 1970 lakini wakapoteza zote.

Kidogo kidogo timu hiyo ikaanza kuanguka kwani 1972 waliishia nusu fainali na baada ya hapo hali ikawa mbaya zaidi.


ANGUKO LA KWANZA
Hawakushiriki tena klabu bingwa Afrika hadi 1977 waliporudi na kuishia raundi ya kwanza baada ya hapo hawakurudi tena hadi 1988...baada ya hapo hawakurudi tena kwenye klabu bingwa hadi 2001.

Kupotea kwenye klabu bingwa kukawapeleka kwenye kombe la washindi ambapo walishinda ubingwa mwaka 1980.

Baada ya hapo, TP Mazembe ikapotea Afrika, hadi 2000 iliporudi kwenye kombe la CAF.

Katika toleo lijalo la makala hii, tutakuletea sababu ya anguko la kwanza lililoanzia miaka ya 1970 na kuendelea hadi miaka ya mwanzo ya 2000 kabla ya kuanza kuangalia ujio wa pili wa kishondo miaka ya 2010.
Inaendelea kesho Jumanne..