Majiha apima afya, kutetea ubingwa wa WBC Afrika

Muktasari:
- Majiha atapanda ulingoni kutetea mkanda wake wa ubingwa wa WBC Afrika katika pambano hilo lililoandaliwa na Promosheni ya Kemmon Sports Agency chini ya Saada Salum.
BONDIA wa ngumi za kulipwa Tanzania, Fadhili Majiha leo amekamilisha zoezi la kupima afya tayari kwa pambano lake la kutetea Mkanda wa Ubingwa wa WBC Afrika dhidi ya Sabelo Ngebinyana kutoka Afrika Kusini, pambano litakalofanyika Julai 20, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mbeya Pub jijini Mbeya.
Majiha atapanda ulingoni kutetea mkanda wake wa ubingwa wa WBC Afrika katika pambano hilo lililoandaliwa na Promosheni ya Kemmon Sports Agency chini ya Saada Salum.
Akizungumza mara baada ya kukamilisha vipimo chini ya Daktari wa Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Dkt. Hadija Hamisi, Majiha alisema mpaka sasa kwa upande wake anamshukuru Mungu kwani anaendelea vizuri na maandalizi kabla ya kueleka jijini Mbeya kukamlisha maandalizi yake.
“Nashukuru Mungu naendelea vizuri na maandalizi yangu, leo nimekamilisha vipimo vya Afya, kesho nategemea nitakuwa Mbeya kuendelea na maandalizi ya mwisho.
“Sabelo ameshakuja hapa Bongo, hivyo siyo mgeni lakini naamini hajapigwa kama nitakavyompiga kwa sababu aliocheza nao hawakumpiga vizuri, naomba wakazi wa Mbeya na mikoa jirani wajitokeze kwa wingi kushuhudia nitakachomfanya bondia huyu wa Afrika Kusini,” alisema Majiha.
Kwa upande wa daktari wa Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Dkt. Hadija Hamisi amefunguka kwamba wamekamilisha zoezi la kisheria kwa mabondia wote wanaotarajia kupanda ulingoni siku hiyo lengo likiwa ni kulinda afya zao.
Majiha alishinda mkanda wa ubingwa huo mwaka jana akimchapa kwa pointi Bongani Mahlangu kutoka Afrika Kusini.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Majiha aliyeanza ngumi mwaka 2008, amepanda ulingoni mara 50, akishinda mapambano 32, kati ya hayo 15 kwa KO, huku akipoteza mapambano 14, matatu yakiwa KO, sare nne.
Mpinzania wake Sabelo Ngebinyana, amepanda ulingoni mara 25, akishinda mapambano 15 huku 11 yakiwa KO, amepoteza nane ambapo mawili KO, sare ni mbili.
Mapambano mengine ambayo ni ya utangulizi siku hiyo yatakuwa hivi; Abeid Zugo vs Ayobonga Sonjica wa Afrika Kusini, Idd Pialali vs Kiaku Ngoy wa DR Congo, Emmanueli Mwakyembe vs Gabriel Ochieng kutoka Kenya, Mubaraka Denso vs George Kandulo kutoka Malawi, Nassibu Habibu vs Ally Lubanja, Daima Bashiru vs Abdallah Zamba na Benjamin Mchunguzi vs Nicolaus Mdoe.