Mkosa, Ebongo wawa kivutio BDL

Muktasari:
- Wachezaji hao wote wanacheza nafasi ya namba 4 “Power Forward” na uwezo wao unafanana na kuwavutia mashabiki wanaohudhuria mechi hizo.
WAKATI Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) ikizidi kushika kasi, nyota wa timu mbili tofauti, Amin Mkosa wa Dar City na Mikado Ebengo wa DSM Outsiders wameonekana kuwa kivutio katika Ligi hiyo.
Kivutio cha wachezaji hao, imetokana na uwezo wa kucheza vizuri katika nafasi wanazocheza na kuzibeba timu zao.
Wachezaji hao wote wanacheza nafasi ya namba 4 “Power Forward” na uwezo wao unafanana na kuwavutia mashabiki wanaohudhuria mechi hizo.
Kwa upande wa Mkosa, mbali ya kucheza nafasi ya namba 4 (Power forward), katika michezo miwili aliyocheza alionekana kumudu kucheza nafasi zote uwanjani.
Nafasi hizo ni ya namba 1 (Point Guard), namba 4 (Shooting Guard), namba 3 (Small Forward), pamoja na namba 5 (Center).
Katika michezo miwili aliocheza ni pamoja na mchezo dhidi ya Pazi, katika mchezo huo Dar City ilishinda kwa pointi 62-47 wakati mchezo wa pili ikaishinda Srelio kwa pointi 105-32
Mkosa aliiambia Mwanaspoti, sababu zilizomfanya acheze nafasi nyingi uwanjani, imetokana na tabia yake ya kutopenda kufungwa.
Kwa upande wa Ebengo mbali ya kucheza namba nne, anacheza pia nafasi ya namba 5 (Center).