Madina, Vicky waiona neema Kenya Ladies Open

Muktasari:
- Mashindano hayo ya siku tatu yatapigwa katika mashimo 54, kila siku yakichezwa mashimo 18, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Chama cha Gofu ya Wanawake Kenya (KLGU).
WAKIWA na ari ya ushindi, Watanzania Madina Iddi na Vicky Elias wamesema wanaiona neema katika mashindano ya wazi ya gofu ya wanawake Kenya ambayo yananza kesho katika viwanja vya Sigona jijini Nairobi.
Mashindano hayo ya siku tatu yatapigwa katika mashimo 54, kila siku yakichezwa mashimo 18, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Chama cha Gofu ya Wanawake Kenya (KLGU).
“Tumewasili salama na tumefanya mazoezi ya kutosha ili kuzifahamu changamoto za viwanja vya Klabu ya Sigona. Naamini mambo yatakuwa mazuri zaidi safari hii,” alisema Madina ambaye anatokea Klabu ya Gymkhana - Arusha.
Vicky Elias ambaye alitarajia kuondoka juzi Jumanne, ataungana na Madina jijini Nairobi na kufanya Tanzania kuwa na wachezaji wawili katika mashindano hayo.
Wakiwa Nairobi, Madina na Vicky watakuwa wakipimana ubavu na wacheza gofu nyota kutoka sehemu mbalimbali za Afrika.
“Naamini upinzani mkubwa zaidi utatoka Kenya ambako kuna wachezaji wengi wenye viwango bora vya gofu barani Afrika,” alisema Madina.
Wote wawili wanarudi tena Kenya baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya wazi ya wanawake yaliyochezwa majuma kadhaa yaliyopita katika viwanja vya Ruiru vya jijini Nairobi.
Kwa Wakenya, Madina ndiye tishio kwao baada ya kumaliza katika nafasi ya pili licha ya kuongoza katika mashimo 36 ya kwanza.
Madina alimaliza katika nafasi ya pili kwa wastani wa mikwaju +8 akiwa nyuma ya mshindi Joyce Wanjiru wa Kenya kwa mkwaju mmoja.
Madina aliliambia gazeti la Mwanaspoti kuwa amepania kuchukua nafasi ya kwanza baada ya kuukosa ubingwa wa michuano ya Ruiru.