Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Machozi ya Okwi na uchawi wa Loga

kocha wa Simba, Zdravko Logarusic.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Yanga waliingia uwanjani kwa ajili ya kufunga mabao na si kufungwa mabao. Walijiamini kama mashabiki wao waliojazana jukwaani. Kwa maana hiyo, umakini wa Kelvin Yondan na Nadir Cannavaro ukapotea kama ulivyopotea katika kipindi cha pili cha pambano lililopita.

SAA 9:20 alasiri juzi Jumamosi, Emmanuel Okwi, alikuwa akiuzunguka Uwanja wa Taifa upande wa Kusini jijini Dar es Salaam akiwapigia makofi mashabiki wa Yanga na kuzusha hisia kali za furaha miongoni mwa mashabiki hao. Mashabiki wa Simba walikuwa wamenywea wakishindwa kuamini macho yao.

Maisha yalienda haraka sana. Saa 12:05 jioni yake, mwamuzi Ramadhan Ibada, alikuwa akimaliza pambano la Nani Mtani Jembe. Ni wachezaji wa Simba ndio waliokuwa wanazunguka uwanja wakishangilia, tena nusu yao wakiwa wamevaa jezi za Yanga. Safari hii ilikuwa zamu ya mashabiki wa Yanga kutoamini macho yao.

Ungesema nini zaidi? Ilikuwa siku ya Simba. Yanga walikuwa wamefanya sherehe yao mapema mwanzoni mwa wiki wakati Okwi alipotua Uwanja wa Ndege na kujiunga na Yanga. Kilikuwa kisu cha moyo, lakini kocha wa Simba, Zdravko Logarusic, alikuwa amewaandalia zawadi nzuri mashabiki wa Simba.

Logarusic alivyowaroga Yanga

Kocha huyu maarufu kwa jina la Loga ndiye aliyewaua Yanga. Amewafanyia kitu kibaya ambacho kinawafanya mashabiki wa Yanga wasijue ni kitu gani kiliikumba timu yao.

Nadhani aliwasoma Yanga katika mikanda au katika pambano dhidi ya KMKM akajua jinsi ambavyo Yanga wana uhatari mkubwa katika eneo la mwisho wakitegemea zaidi kasi ya Mrisho Ngassa na Simon Msuva.

Alichofanya Loga kilikuwa kitu rahisi. Katika uwanja kuna maeneo makubwa matatu. Eneo lako la nyuma, eneo la katikati na eneo la ushambuliaji. Loga alifahamu kuwa ingekuwa hatari kwa timu yake kuanza kuwakaba Yanga katika eneo la katikati.

Ukiwakaba Yanga katika eneo la katikati huwa wanafurahi kwa sababu viungo wao, hasa Athuman Idd ‘Chuji’ hupenda zaidi kuvusha mpira nyuma ya ukuta wa timu pinzani na kuruhusu eneo kubwa kwa Msuva na Ngassa kukimbia.

Loga alichofanya ni kuhakikisha kuwa mabeki wake wanakabia katika eneo lao la nyuma kabisa na kutowaruhusu hata walinzi wa pembeni, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Haruna Shamte ‘Terminator’ kutopanda mbele. Kiaina Simba wakawa wamepaki basi lao vizuri. Muda mwingi Yanga walimiliki mpira eneo fulani la katikati, lakini hakukuwa na nafasi yoyote ambayo wangeweza kuuvusha mpira nyuma ya walinzi wa Simba na kumfanya Ngassa akimbie kwa sababu tayari walinzi wa Simba walikuwa nyuma.

Katika hali kama hii, maisha yanakuwa magumu kwa timu zote zinazopenda soka la namna hii kama Barcelona na Arsenal. Anahitajika fundi wa kuweza kupenyeza mipira katika msitu wa walinzi. Kwa sababu mchezaji huyo hayupo Simba, Azam, Yanga wala timu ya taifa. Yupo Coastal Union ya Tanga. Anaitwa Haruna Moshi ‘Boban’.

Ndio maana katika kipindi cha kwanza Yanga walionekana kuwa na mpira wao wakati fulani, lakini hawakujua wapenye vipi. Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa, Hamis Kiiza aliyecheza pembeni kushoto wote walishindwa kumfikia kwa haraka mlengwa, Didier Kavumbagu kwa sababu mbele yao kulisimama msitu mrefu ulioanzia kwa Jonas Mkude.

Tambwe na mabao yake

Yanga waliingia uwanjani kwa ajili ya kufunga mabao na si kufungwa mabao. Walijiamini kama mashabiki wao waliojazana jukwaani. Kwa maana hiyo, umakini wa Kelvin Yondan na Nadir Cannavaro ukapotea kama ulivyopotea katika kipindi cha pili cha pambano lililopita.

Bao la kwanza la Simba lilikuja kwa kazi nzuri ya Henry Joseph kuubetua mpira juu ya walinzi wa Yanga. Ukaunganishwa na Haroun Chanongo ambaye alikabwa kwa pamoja na Yondani na Cannavaro huku Tambwe akiwa peke yake.

Ilikuwa kazi rahisi kwa Tambwe kuuweka mpira wavuni wakati anatazama na Juma Kaseja. Ilikuwa rahisi kuliko kupaka siagi katika mkate au baunsa kunyanyua kikombe la chai.

Yanga walipata hasira, lakini haikuwasaidia. Kadiri walivyokwenda mbele ndivyo walivyopishana na Simba. Ilikuwa hatari kwao. Walikuwa wanaondoka wengi nyuma kwa mpigo. Loga aliwatuliza vijana wake kwa ajili ya mashambulizi ya kushtukiza. Nusura Haruna Chanongo aipatie Simba bao kama si kukosa umakini wakati alipotazamana na Juma Kaseja akiwa na mpira upande wa Mashariki.

Baadaye kidogo, mpira ulipokuja upande wa Magharibiki karibu kabisa na eneo ambalo Okwi alikuwa anawapigia makofi mashabiki wa Yanga kabla mechi haijaanza, Ramadhan Singano ‘Messi’ alijikuta akitazamana peke yake na David Luhende.

Ilikuwa kazi rahisi kwa Messi ambaye anaimarika kila siku. Ana kasi, chenga na akili. Alimtoka Luhende na kupigwa mtama. Ilikuwa penalti ambayo hata wanafunzi wanaosomea uamuzi wangeitoa kirahisi.

Wakati Tambwe akienda kupiga, kocha Loga hakutazama penalti hiyo. Alikuwa anawatazama mashabiki wa Simba. Kelele zao za kushangilia baada ya Tambwe kufunga ndizo zilimuashiria kuwa alikuwa amemaliza kazi na wala hakulihitaji bao la zawadi la Kaseja katika kipindi cha pili.

Brandts, Basi lilishindwa na ndege ikashindwa

Kama ilivyo kwa makocha wengi wa staili ya soka la Yanga katika kipindi cha kwanza. Walipochemsha katika mipira ya chini, kocha Ernie Brandts akaingia mpango wa pili (Plan B) wa kupiga krosi na kutegemea mipira ya kurushwa ya Mbuyu Twite. Haikusaidia.

Ivo Mapunda alikuwa katika ubora wake kama ilivyokuwa katika mechi za Chalenji. Ivo huyu si yule wa siku zile. Huyu akikamata mpira haumtoki. Huyu ana ‘timing’ katika mipira ya krosi.

Lakini zaidi ya yote, kiboko wa Yanga alikuwa Waziri wa Ulinzi katika safu ya Simba, Mkenya Donald Musoti. Alicheza mipira yote ya hewani. Alifagia mipira yote ya chini. Ilikuwa kama vile anacheza peke yake katika safu ya ulinzi ya Simba.

Kaseja, siku ya kufa nyani

Hakuna kipa ambaye miguu yake inafanya kazi vizuri kama Juma Kaseja. Hata akicheza ndani hakuna tatizo. Lakini alikuwa anafikiria nini alipofungwa bao la tatu? Atajiuliza kwa maisha yake yote, na wakati mwingine anaweza pia kumuuliza mkewe, Nasra Nassor nini kilitokea?

Juma alikuwa na mawazo mawili aliporudishiwa mpira na Yondani. Kwa sababu alikuwa nje ya boski, alitaka aukokote kwa haraka aingie nao ndani ya boksi na kuudaka. Akagundua lingekuwa kosa. Akataka ampige chenga Awadhi Juma akachemsha. Akaugonga, ukasogea mbele, Awadhi akautokea na kufunga.

Kosa la kibinadamu na akina Iker Casillas pia huwa wanafanya. Usiwe mwanzo wa maneno kwa sababu Juma alikuwa katika lango la Yanga, katika jezi ya njano na kijani.

Bao la Okwi lilikuja wakati nusu ya mashabiki wa Yanga wakiwa wakibishana na makonda katika daladala. Na lilitokana na kosa pekee ambalo safu ya ulinzi ya Simba walilifanya dakika 90 za mchezo huo! Lakini walau lilimfariji Okwi na tajiri wake, Abdallah Bin Kleib kuwa pesa yake imeanza kurudi.