Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabao ya kuvutia zaidi mechi za fainali Ulaya

Muktasari:

  • Bao ambalo lilikuwa na thamani ya kuwa bao la ushindi kwa mechi yoyote ya soka ile achilia mbali pambano la fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Zizou ambaye kwa sasa ni kocha wa Bale, alifunga bao hilo akiusubiri mpira wa hewani kabla haujatua na mpira ulikwenda moja kwa moja wavuni kwa Leverkusen. Zidane alikuwa dhahabu katika kizazi cha Magalactico na katika mechi hii alithibitisha thamani yake.

JUMAMOSI usiku, staa wa Real Madrid, Gareth Bale alifunga bao ambalo liliwaacha mdomo wazi mashabiki wa soka waliokuwa wakifuatilia pambano la fainali kati ya Real Madrid na Liverpool pale Kiev. Hili linakuwa moja kati ya mabao ya kusisimua ya pambano la fainali za Ulaya. Mengine haya hapa.

Zinedine Zidane (Real Madrid v Bayer Leverkusen, 2002)

Bao ambalo lilikuwa na thamani ya kuwa bao la ushindi kwa mechi yoyote ya soka ile achilia mbali pambano la fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Zizou ambaye kwa sasa ni kocha wa Bale, alifunga bao hilo akiusubiri mpira wa hewani kabla haujatua na mpira ulikwenda moja kwa moja wavuni kwa Leverkusen. Zidane alikuwa dhahabu katika kizazi cha Magalactico na katika mechi hii alithibitisha thamani yake.

Ole Gunnar Solskjaer (Man United vs Bayern, 1999)

Linaweza lisiwe bao zuri sana lakini lilifungwa wakati muhimu na katika mech muhimu. Bao hili dhidi ya kipa mkongwe wa Bayern Munich, Oliver Kahn linabakia kuwa moja kati ya mabao bora zaidi katika historia ya mechi za fainali. Alimalizia vema kona ya David Beckham kabla ya Teddy Sheringham kufunga bao la pili ambalo liliipa ubingwa wa ajabu Manchester United iliyokuwa chini ya Sir Alex Ferguson.

Mario Mandzukic (Juventus vs Real Madrid, 2017)

Juventus ina rekodi mbovu katika mechi za fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ukijumlisha fainali ya msimu uliopita dhidi ya Real Madrid amnbapo ilichapwa mabao 4-1. Pamoja na kichapo hicho cha Juventus, pambano hilo linakumbukwa kwa bao maridadi la kusawazisha la mshambuliaji wa kimataifa wa Croatia, Mario Mandzukic.

Alituliza mpira wa juu akauweka kifuani kabla ya kuunganisha vizuri akigeuka hewani na mpira ukampita kipa, Keylor Navas. Bahati mbaya kwa Vibibi Vizee vya Turin, walichapwa mabao mengi.

Didier Drogba (Chelsea v

Bayern Munich, 2012)

Kama kulikuwa na mchezaji ambaye alikuwa anasubiri mechi kubwa basi ni Didier Drogba. Huku mechi hii iliyochezwa katika uwanja wa wenyeji ikielekea ukingoni na Bayern Munich ikiongoza bao 1-0, Chelsea ilipata kona katika dakika ya 88 ambayo ilipigwa na Juan Mata kabla ya kumaliziwa vema na staa huyu wa kimataifa wa Ivory Coast huku kipa hodari, Manuel Neuer akiwa hana la kufanya. Drogba pia ndiye aliyemalizia penalti ya mwisho ambayo iliipatia Chelsea ubingwa wa Ulaya mwaka huo na hivyo kuwa timu ya kwanza ya London kuchukua ubingwa wa Ulaya.

Hernan Crespo (AC Milan v Liverpool, 2005)

Kwa jinsi ambavyo fainali ya mwaka 2005 ilivyokwenda na wachezaji wa Liverpool kuibuka mashujaa, basi ni rahisi sana kusahau bao liliofungwa na staa huyu wa kimataifa wa Argentina. Crespo aliunyanyua mpira kwa umaridadi mkubwa na kumvuka kipa wa Poland, Jerzy Dudek baada ya kupokea pasi ndefu kutoka kwa Kaka. Lilikuwa bao la tatu ambalo lilionekana kama vile lilikuwa linaihakikishia ushindi AC Milan lakini Liverpool ikapindua matokeo.

Lars Ricken (Borussia Dortmund vs Juventus, 1997)

Lars Ricken ni mkongwe anayeheshimika Borussia Dortmund, shukrani zaidi kwa bao hili maridadi la ushindi alilofunga dhidi ya Juventus katika pambano la fainali Ligi ya Mabingwa mwaka 1997. Aliingia akitokea katika benchi na kukutana na mpira nje ya boksi. Ilidhaniwa angeweza kuendelea kuufanyia jambo lakini akaunyanyua kwa umaridadi bila ya kipa wa Juventus na mashabiki kutazamia. Kwa wakati huo, hilo lilikuwa bao la haraka zaidi katika historia kwa mchezaji ambaye alikuwa ametokea benchi.

Diego Milito (Inter Milan vs Bayern Munich, 2010)

Diego Milito alikuwa na kipindi kizuri chini ya Kocha Jose Mourinho kiasi kwamba kila alichogusa kiligeuka kuwa bao. Muargentina huyu aliongoza vita dhidi ya Bayern Munich katika pambano la fainali za mwaka 2010 akifunga mabao mawili katika pambano hilo huku Inter Milan ikiondoka na mataji matatu. Bao lake la pili lilikuwa zuri akipokea pasi maridadi kabla ya kufunga kwa urahisi karibu kabisa na lango la Bayern.

Steve McManaman (Real Madrid v Valencia, 2000)

Wachezaji wengi wa Kiingereza wamewahi kutamba katika jezi nyeupe ya Real Madrid lakini kiungo wa zamani wa Liverpool, Steve McManaman alikuwa mmoja kati ya wachezaji wa mwanzo kufanya hivyo. Katika fainali za mwaka 2000 dhidi ya Valencia, staa huyu aliufumania mpira nje ya boksi la Valencia na kupiga shuti la karate ambalo lilikwenda moja kwa moja nyavuni na kuipa Madrid ushindi wa mabao 3-0. Bao murua katika wakati murua.

David Villa (Barcelona vs Manchester United, 2011)

Hata Sir Alex Ferguson na watukutu wake wa Manchester waliwahi kushindwa kuzuia pasi za Pep Guardiola maarufu kama tiki-taka. Ilikuwa wakati huo Barcelona ikiwa katika ubora wake na United ilijipendekeza vema katika pambano hili la fainali mwaka 2011 jijini London katika Uwanja wa Wembley. David Villa akiwa amesimama nje ya boksi alipokea pasi murua na kupiga shuti zuri la kukata ambalo lilikwenda moja kwa moja katika nyavu za kipa mkongwe wa Kidachi, Edwin van der Sar ambaye hakujua namna ya kufanya.

Dejan Savicevic (AC Milan vs Barcelona, 1994)

Kwa sasa AC Milan imebakia kuwa katika kivuli tu cha timu yao ya zamani ambayo iliwahi kutamba mwishoni mwa miaka ya 1980 na 1990 na kisha katikati ya miaka ya 2000. Katika moja kati ya fainali za miaka hiyo wakati wanatesa waliwahi kuiadhibu Barcelona mabao 4-1. Usiku huo, lilikuwa moja kati ya mabao ya kuvutia lilikuwa la staa huyu wa zamani wa Yugoslavia, Dejan Savicevic aliyepokea mpira nje ya boksi kando akaunyanyua mpira kwa umaridadi mkubwa na ukatinga wavuni kwa mvuto wa aina yake.

Gareth Bale (Real Madrid vs Liverpool, 2018)

Linaweza kuwa bao bora zaidi katika historia ya mechi za fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Lilifungwa Jumamosi usiku baada ya Gale kupokea pasi safi ya Marcelo. Alijinyanyua hewani na kupiga tik-taka ya aina yake ambayo licha ya uzembe wa kipa wa Liverpool, Loris Karius siku hiyo lakini usingeweza kumlaumu kwa bao hilo. Bao bora sana.