Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabao ya kukumbukwa fainali za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya

FAINALI ya ubingwa wa Ulaya imekaribia. Ni Liverpool dhidi ya Real Madrid pale Kiev. Wakati mwingine pambano kama hili hutoa mabao ya kusisimua ambayo yanakumbukwa kwa muda mrefu na mashabiki. Yafuatayo yanaweza kuwa mabao ya kukumbukwa zaidi katika mechi za ubingwa wa Ulaya.

Zinedine Zidane (Real Madrid v Bayer Leverkusen, 2002)

Bao ambalo lilikuwa na thamani ya kushinda mechi yoyote ile ya soka achilia mbali pambano la fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Katika pambano hili lililochezwa Scotland, Zidane aliusubiri mpira unaotua na kuungusha kwa shuti kali la moja kwa moja na kufunga bao ambalo kwa muda mrefu sasa limekuwa likikumbukwa na mashabiki wa soka.

Ole Gunnar Solskjaer

Linaweza lisiwe bao bora kwa maana ya namna lililovyofungwa, lakini kwa jinsi lilivyofungwa katika dakika muhimu, linabakia kuwa moja kati ya mabao ya kukumbukwa katika fainali kama hizi. Staa huyu wa kimataifa wa Norway katika dakika za mwishoni akimalizia kona ya David Beckham katika pambano hili dhidi ya Bayern Munich pale Nou Camp. Linabakia kuwa moja kati ya mabao ya kukumbukwa katika historia huku likimpatia Sir Alex ferguson taji lake la kwanza la Ulaya.

Mario Mandzukic (Juventus vs Real Madrid, 2017)

Juventus ina rekodi mbovu katika mechi hizi za fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Imepoteza fainali saba ikiwemo ya mwaka uliopita wakati walipochapwa na Real Madrid mabao 4-1. Pamoja na kichapo hicho lakini mshambuliaji wa kimataifa wa Croatia wa Juventus, Mario Mandzukic alifunga moja kati ya mabao ya kukumbukwa ya mechi za fainali. Baada ya pasi za hapa na pale kutoka kwa Juventus, mshambuliaji wa Argentina, Gonzalo Higuain alimtulizia mpira Mandzukic kwa kifua na staa huyu akajipindua hewana na kupiga Tik Tak akimfunga vizuri kipa, Keylor Navas. Bahati mbaya bao hilo halikuweza kuwatia nguvu Juventus kuanza kurudisha mabao na kuchukua ubingwa.

Didier Drogba (Chelsea v Bayern Munich, 2012)

Kama kuna mchezaji ambaye alikuwa tayari siku zote kwa ajili ya mechi kubwa basi ni Didier Drogba. Huku Chelsea ikielekea kupoteza pambano la fainali dhidi ya Bayern Munich mwaka 2012 katika Uwanja wa Bayern Munich, Allianz Arena, Drogba aliunganisha kwa nguvu kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Juan Mata na kumpita kipa mahiri, Manuel Neurer aliyekuwa amesimama katika mwamba wake. Pambano lilikwenda katika dakika za nyongeza kisha mikwaju ya penalti ambapo Drogba alifunga penalti ya ushindi iliyowapa Chelsea taji lao la kwanza la ubingwa wa Ulaya.

Hernan Crespo (AC Milan v Liverpool, 2005)

Kutokana na ushujaa mkubwa ulionyeshwa na mastaa wa Liverpool katika kipindi cha pili cha fainali hii ya kukumbukwa ya ubingwa wa Ulaya 2005, ni rahisi sana kusahau bao zuri lililofungwa na staa wa kimataifa wa Argentina wa AC Milan, Hernan Crespo. Alipenyezewa mpira mzuri na kiungo wa Brazil, Kaka na kujikuta akitazamana na kipa wa Liverpool, Jerzy Dudek. Aliubetua vema mpira huo juu ya nywele za Dudek na kutingisha nyavu za Liverpool. ingawa lilikuwa bao la tatu, lakini halikutosha kuwapa ubingwa AC Milan baada ya Liverpool kukomboa mabao yote.

Lars Ricken (Borussia Dortmund vs Juventus, 1997)

Lars Ricken ni mmoja kati ya mastaa wa zamani wanaoheshimika Borussia Dortmund, shukrani kubwa kwa bao la kuvutia katika fainali za Ulaya za mwaka 1997 dhidi ya Juventus. Alikuwa ameingia uwanjani sekunde 16 tu zilizotangulia na akapenyezewa mpira mzuri ambao awali alionekana kama vile alikuwa ana nafasi ya kuukimbiza, lakini akaamua kuunyanyua juu moja kwa moja juu ya kipa wa Juventus ambaye hakuwa na kufanya zaidi ya kuutazama mpira ukitinga wavuni. Kwa wakati huo lilikuwa limeweka rekodi ya kuwa bao la haraka zaidi kufungwa na mchezaji aliyetokea benchi.

Diego Milito (Inter Milan vs Bayern Munich, 2010)

Diego Milito alikuwa na nyakati nzuri chini ya kocha, Jose Mourinho kiasi kwamba kila alichogusa kiligeuka kuwa dhahabu. Katika pambano la fainali za mwaka 2010 dhidi ya Bayern Munich aliwahenyesha vilivyo Bayern Munich huku akifunga mabao mawili na kuipa Inter ubingwa. Bao la pili la Muargentina huyo lilikuwa tamu baada ya kumkimbiza beki mmoja wa Bayern na kumpiga chenga kabla ya kupiga shuti zuri lililokwenda wavuni.

Steve McManaman (Real Madrid v Valencia, 2000)

Wachezaji kadhaa wa Kiingereza wamewahi kutamba katika jezi ya Real Madrid, lakini kiungo wa zamani wa Liverpool, Steve McManaman alikuwa mchezaji wa kwanza kufanya hivyo. Katika fainali dhidi ya Valencia mwaka 2000 aliusubiri mpira katika mstari wa boksi la adui na kupiga shuti la karate ambalo lilimshinda kipa wa Valencia. Usiku huo Madrid waliiadhibu Valencia mabao 3-0.

David Villa (Barcelona vs Manchester United, 2011)

Hata Sir Alex Fergsuon alishindwa kuzuia pasi za Tiki-Taka za kocha, Pep Guardiola wakati akiwa na Barcelona. Katika fainali hii ya mwaka 2011 iliyopigwa Wembley, United walizidiwa kwa kiasi kikubwa huku wakichapwa mabao 3-1. Moja kati ya mabao hayo ni bao zuri lililofungwa na mshambuliaji, David Villa aliyemchungulia kipa, Edwin van der Sar na kuukata mpira mrefu uliotinga nyavu za juu. Hata kama kipa huyu wa Kidachi asingeruka bado asingeweza kulaumiwa. Makipa wawili kwa pamoja wasingeweza pia kuzuia bao hilo.

Dejan Savicevic (AC Milan vs Barcelona, 1994)

AC Milan imebakia katika kivuli cha timu iliyotamba Ulaya kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1980 mpaka mwanzoni mwa miaka ya 2000. Moja kati ya viwango bora ilivyowahi kutoa ni katika pambano la ubingwa wa Ulaya mwaka 1994 dhidi ya Barcelona ambapo walishinda 4-1. Moja kati ya bao la kuvutia ni la Dejan Savicevic aliyeunyayua kwa umaridadi mkubwa mpira alioupora kulia mwa uwanja na kuupiga kabla hajafikia boksi la Barcelona. Lilikuwa bao zuri.