Maana 10 za picha hii

JANA, nyota wanne wa Simba na Yanga, Clatous Chama, Henock Inonga, Kennedy Musonda na Fiston Mayele walipiga picha ya pamoja walipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Addis Ababa, Ethiopia ambako waliunganisha ndege kwenda Zambia na DR Congo kujiunga na timu zao za taifa.

Picha hiyo imekuwa gumzo kutokana na ustaa wa nyota hao kwenye timu zao ambazo ni watani wa jadi lakini wenyewe wakaonyesha kwa vitendo namna soka ulivyo ni mchezo wa kiungwana kwa kuweka pembeni tofauti zao za kitimu na kuonyesha urafiki.

Ni picha ambayo inaweza kuzungumza vitu vingi lakini kati ya hivyo vipo 10 ambavyo picha hiyo ya pamoja ya Musonda, Inonga, Chama na Mayele inaweza kuvizungumza;


1. Roho za Simba na Yanga. Ni picha inayoonyesha mastaa wanne ambao wamekuwa uti wa mgongo wa timu zao. Inonga ni tegemeo kwenye safu ya ulinzi ya Simba huku Chama akiwa muhimili katika safu ya kiungo. Kwa upande wa Mayele na Musonda, wamekuwa tegemeo katika safu ya ushambuliaji ya Yanga.


2. Matumizi sahihi ya Dirisha Dogo. Ni picha inayomjumuisha Kennedy Musonda ambaye tangu alipojiunga na Yanga katika dirisha dogo msimu huu, hajawaangusha waliomsajili na amefumania nyavu mara tatu katika mechi tano za hatua ya makundi na kuivusha Yanga.


3. Picha ya mabao. Ni picha inayoonyesha wachezaji wanne waliohusika na idadi kubwa ya mabao katika timu zao kwenye hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika. Kati ya mabao 17 yaliyofungwa na Yanga na Simba kwenye hatua ya makundi, wanne hao wamehusika na mabao 15. Wameziheshimisha Simba na Yanga.


4. Wazambia tishio. Chama na Musonda walio katika picha hiyo ni wachezaji wawili ambao kila mmoja anaongoza kwa kuhusika na mabao mengi kwenye mashindano hayo ya klabu Afrika kulinganisha na wachezaji wengine wa timu mbalimbali. Chama katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa anaongoza akiwa amehusika na mabao matano kama ilivyo kwa Musonda anayeongoza kwenye Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na mabao matano pia.


5. Heshima kwa Tanzania. Ni picha inayohusisha wachezaji wanne wanaong’ara katika Ligi Kuu ya NBC ambao ni miongoni mwa nyota wachache wanaocheza soka ndani ya Afrika kuitwa katika timu zao za taifa yaani DR Congo na Zambia.


6. Utani siyo Uadui. Chama, Mayele, Musonda na Inonga wamepiga picha inayokumbusha kuwa upinzani wa wachezaji huishia ndani ya uwanja. Nje ya uwanja ni marafiki wakubwa jambo ambalo hata mashabiki wa Simba na Yanga wanapaswa kujifunza.


7. Wakali wa Ligi Kuu. Ni picha inayohusisha wachezaji wawili wanaotamba katika Ligi Kuu msimu huu. Mayele ndio kinara wa ufungaji akiwa amepachika mabao 15 wakati Chama ndiye anaongoza kwa kupiga pasi nyingi za mwisho akiwa nazo 15.


8. Vipenzi vya mashabiki. Ni nyota wanne ambao wamekuwa vipenzi vya mashabiki kwenye klabu zao kutokana na kiwango bora wanachokionyesha uwanjani.


9. Chama haringi. Ni picha ambayo kuna mchezaji aliyeingia katika 10 bora ya wafungaji bora wa muda wote wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Clatous Chama ambaye amefumania nyavu mara 19 katika mashindano hayo na wala haringi.


10. Jeuri ya Pesa. Hawa mastaa wanalipwa kiasi kikubwa cha fedha kwenye timu zao kulinganisha na wachezaji wengine wanaocheza katika nafasi zao na thamani yao imeonekana miguuni.