Lwanga gari limewaka

Wednesday October 20 2021
LWANGA PIC

BAADA ya juzi kuwa sehemu ya ushindi wa Simba wa mabao 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy, kiungo mkabaji Thadeo Lwanga ameeleza furaha yake baada ya kupata matokeo katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lwanga aliipatia Simba bao la kuongoza katika dakika ya pili ya mchezo huo uliopigwa mjini Gaborone baada ya mabeki kuzubaa kuondoa mpira wa kona uliopigwa na Rally Bwalya na sasa Wekundu wa Msimbazi wanajipanga kumaliza kazi katika mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam Jumapili hii.

Kiungo huyo Raia wa Uganda alisema anaamini ataendelea kufunga na kuisaidia timu yake kupata matokeo endapo atapata nafasi ya kufanya hivyo.

“Kama mchezaji najisikia furaha sana kufunga kwenye michuano mikubwa kama hii na kuisaidia timu yangu kupata ushindi ugenini, binafsi naamini nitaendelea kufunga kama nikipata nafasi ya kufanya hivyo,” alisema Lwanga, ambaye hili ni bao lake la pili tangu ajiunge na timu hiyo Januari mwaka huu, baada ya lile la awali kuipa Simba ubingwa wa Kombe la Shirikisho (ASFC) walipowalaza mahasimu wao Yanga 1-0 katika fainali msimu uliopita.

Aidha, Lwanga alisema licha ya kuwa na mtaji mzuri wa mabao hayo ya ugenini hawatakiwi kuwachukulia poa Jwaneng Jumapili.

Advertisement