Lokosa: AS Vita kazi wanayo leo

Kinshasa. Mshambuliaji mpya wa Simba, Junior Lokosa, ambaye amesajiliwa kwa mkataba wa miezi sita wa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika anaweza kukosekana katika mechi ya mzunguko wa kwanza hatua ya makundi dhidi ya AS Vita.
Katika mazoezi ya Simba ambayo yalifanyika Kinshasa, Lokosa aliondolewa katika mipango ya wachezaji ambao watakwenda kucheza mechi hiyo na alifanya mazoezi mengi ya binafsi.
Mazoezi ya kwanza ambayo Simba walifanya katika Uwanja wa Martyrs, juzi, kuanzia saa 2:00 ya hapa Kinshasa. Lokosa na washambuliaji wengine wote walikuwa wakifanya mazoezi mbalimbali ya kupiga mshuti ambayo yalisimamiwa na kocha wa makipa, Mbrazil Milton.
Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, kocha Didier Gomes alisema maandalizi yao yamekwenda vizuri tangu wakiwa Dar es Salaam, kwa ajili ya kuwakabili AS Vita na wana imani watapa matokeo mazuri ambayo wanayahitaji.
“Baada ya kusafiri kwa muda wa siku mbili tumefanya mazoezi yetu ya kwanza leo (Alhamisi), wachezaji wote wameonekana kuwa na morali ya hali ya juu ili kwenda kukipigania kile ambacho wanakihitaji katika mashindano haya.
“Binafsi kwa maandalizi yetu ambayo tumeyafanya hapa Kinshasa na yale ya nyumbani naamni tunaweza kufanya vizuri licha ya kwamba mechi za ugenini zinakuaga na ugumu kutokana na mambo mbalimbali ambayo yanafanyika,” alisema Gomes.
Katika hatua nyingine kinara wa mabao katika kikosi cha Simba, Meddie Kagere alisema wakati wanafungwa mabao 5-0, walikuwa na timu tofauti na aliyokuwepo wakati huu, lakini hata benchi la ufundi limefanyiwa mabadiliko.
Kagere alisema si kama walivyofungwa mabao hayo walikuwa ndiyo basi bali kuna vitu ambavyo walivichukua na wamejifunza na ndiyo watakewenda kuvitumia kwa mara nyingine katika mchezo wa leo.
“Wakati tunakuja kucheza hapa na AS Vita ilikuwa mara ya kwanza kwetu, lakini baada ya kufungwa idadi kubwa ya mabao tumejifunza mambo mengi, hata aina ya mabadiliko ambayo yamefanyika katika benchi la ufundi hatutacheza kama wakati ule,” alisema Kagere, ambaye katika ligi amefunga mabao tisa.