Ligi ya Kikapu Dar ni burudani ndani, nje

Muktasari:
Hilo limetokea kwa timu ya wanawake ya Tausi Royals iliyoshinda kwa pointi 120-25 dhidi ya UDSM Queens, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa DonBosco, Upanga ambapo wakati ulipokuwa unaelekea mwishoni, wachezaji wa timu hiyo walianza kuwapa moyo wapinzani angalau na wao waweze kufunga.
UKIACHANA na ushindani wa uwanjani wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), burudani nyingine ni kutoka kwa mashabiki wa mchezo huo, wanaoweza kufurahia mchezaji wa upinzani pindi anapofanya kitu kizuri.
Hilo limetokea kwa timu ya wanawake ya Tausi Royals iliyoshinda kwa pointi 120-25 dhidi ya UDSM Queens, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa DonBosco, Upanga ambapo wakati ulipokuwa unaelekea mwishoni, wachezaji wa timu hiyo walianza kuwapa moyo wapinzani angalau na wao waweze kufunga.
UDSM Queens ilionekana kuzidiwa kila eneo na Tausi Royals ambayo mashabiki wake walikuwa na shangwe muda wote na mwisho wa yote walianza kuwashangilia na wapinzani pia.
Kitendo cha kufurahishwa na kazi iliyokuwa inafanywa na mpinzani haikuwa kwa Tausi Royals pekee bali hata kwa wachezaji wa UDSM Queens ambao walikuwa benchini, walikuwa wakishangilia pointi zilizokuwa zikifungwa kwa umbali mrefu vya wapinzani wao.
Mchezo mwingine wa wanaume ambao ulianza kuchezwa saa 2:00 usiku baina ya Kurasani Heart iliyopoteza mbele ya Mchenga Stars kwa pointi 65-68, ulikuwa wa ushindani na kutumia nguvu zaidi.
Matokeo yote ya mechi za juzi Alhamisi katika michezo iliyopigwa Uwanja wa Don Bosco, Upanga jijini Dar es Salaam ni Polisi Stars 95-18 Kurasani Divas, Tausi Royals 120-25 UDSM Queens, Kurasani Heat 65-68 Mchenga Stars na Kiut 70-41 Polisi. Ligi hiyo ya kikapu inaendelea tena leo kwenye Viwanja vya DonBosco, Upanga.