Laizer mbioni kurejea Fountain Gate

Muktasari:
- Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimelidokeza Mwanaspoti kuwa, Laizer atakabidhiwa mikoba ya kukiongoza kikosi hicho katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara zilizosalia akiungana na Melis Medo atakayetangazwa kuwa mkurugenzi mpya wa ufundi.
TIMU ya Fountain Gate iko katika hatua za mwishoni za kumrejesha aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Mohammed Ismail ‘Laizer’, huku makocha wa kikosi hicho kwa sasa Khalid Adam na Amri Said ‘Stam’ wakiwa mbioni kuondoka.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimelidokeza Mwanaspoti kuwa, Laizer atakabidhiwa mikoba ya kukiongoza kikosi hicho katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara zilizosalia akiungana na Melis Medo atakayetangazwa kuwa mkurugenzi mpya wa ufundi.
“Medo ameshaanza majukumu yake, lakini sio kocha mkuu yeye atakuwa ni mkurugenzi wa ufundi na Laizer ndiye atakayepewa majukumu ya Khalid Adam na Amri Said ‘Stam’ ambao wataondolewa kwa makubaliano ya pande mbili,” kilisema chanzo kutoka ndani ya timu hiyo.
Kwa upande wake Laizer alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia suala hilo, alisema kwa sasa ni mapema na kama kutakuwa na makubaliano yoyote, basi uongozi wa Fountain Gate utaweka wazi, hivyo hawezi kuzungumzia taarifa zilizopo mitandaoni.
Laizer anarejea katika timu hiyo baada ya awali kuanza nayo msimu akiwa kocha msaidizi wa Mohammed Muya ambapo waliondoshwa Desemba 29, 2024 kwa makubaliano ya pande mbili na klabu hiyo, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuchapwa mabao 5-0 na Yanga. Baada ya hapo ndipo Muya akajiunga na Geita Gold huku Laizer akitua TMA zote zikiwa zinashiriki Ligi ya Championship msimu huu iliyotamatika Mei 11, 2025.
Akiwa na TMA, Laizer alikuwa kocha mkuu baada ya Maka Mwalwisi kuondoka na kujiunga na Mbeya Kwanza, huku akiiwezesha kumaliza nafasi ya tano ikiwa na pointi 53 baada ya kushinda mechi 15, sare nane na kuchapwa saba.
Laizer anatua katika timu hiyo baada ya kuondoka pia kwa aliyekuwa Kocha Mkenya Robert Matano ambapo kikosi hicho kwa sasa kimecheza mechi sita mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ushindi tangu mara ya mwisho kilipoifunga KMC mabao 2-1.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, Machi 6, 2025, ilikuwa ya mwisho kwa kikosi hicho kushinda ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao mawili na kuruhusu nyavu kutikiswa mara 14. Fountain Gate inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 29 Ligi Kuu Bara.