Kwenye gofu ukilala njaa ni uzembe wako

Muktasari:

  • Mzuka wa gofu, kupitia gazeti la Mwanaspoti, limefanya mahojiano na Prosper Emmanuel anayesimulia mishe anazofanya nje na kucheza gofu, zinazompa pesa za kujikimu maisha yake.

KUNA watu wamegundua fursa zilizopo kwenye mchezo wa gofu na wameamua kupiga pesa, kutokana na mishe mbalimbali wanazozifanya, jambo kubwa lililowafanikisha hayo ni uthubutu na kutoona aibu.

Mzuka wa gofu, kupitia gazeti la Mwanaspoti, limefanya mahojiano na Prosper Emmanuel anayesimulia mishe anazofanya nje na kucheza gofu, zinazompa pesa za kujikimu maisha yake.

“Kwanza kama kijana napenda kuthubutu, sipendi uvivu wakati huu ambao nina nguvu za kutafuta maisha, ndiyo maana sijaishia kucheza pekee, nilipogundua kuna vitu vya ziada naweza kufanya vikanipa masilahi, navifanya,” anasema Prosper.


GoFU IMEMBADILISHA

“Kupitia gofu nimekutana na viongozi kutoka serikalini na sekta binafsi na nje ya mchezo huo, isingekuwa rahisi kuonana nao uso kwa uso, najifunza vitu vingi vya kimaisha kutokana na jinsi ninavyozungumza nao,” anasema na kuongeza;

“Nimetembea nchi mbalimbali kama Uganda na Kenya ambako nilikwenda kucheza mashindano binafsi, kwa ufupi mchezo huo umebadilisha maisha yangu kwa asilimia kubwa.”

Ana handcup 4, lakini bado anaendelea kupiga pesa kwa kukedi wachezaji wengine (kuwabebea vifaa), anatumia kama fursa ya kujitengenezea kipato cha kujikimu na maisha yake.

“Mbali na kucheza gofu, unaweza ukabeba vifaa vya wachezaji wenzako wakicheza, ndio maana huwa napenda kuwaambia vijana waachane na maisha ya vijiweni, gofu itabadilisha maisha yao kimtazamo na kiuchumi,” anasema na kuongeza;

“Mimi ni dereva, kuna wakati mwingine viongozi mbalimbali wa hapa Lugalo na kutoka nje ya Lugalo wanaokuja kucheza gofu, nakuwa nawaendesha, najikuta nazidi kujiongezea kipato cha kujikimu na maisha yangu, kwani nina watu wengi wanaonitegemea.

“Ukiingia kwenye gofu huwezi kufa njaa, lazima utakutana na dili mbalimbali za kukupa kipato, ama ukaunganishwa kufanya kazi sehemu fulani, vijana wanachelewa kuona fursa zilizopo kwenye mchezo huo na badala yake wanaishia kulalamika ukata.”

Anasema alianza kufanya kazi ya ukedi mwaka mwaka 2010, hivyo kilichomshawishi ajiunge 2013 ni jinsi marafiki zake walivyokuwa wanacheza na yeye kujua sheria zake, akaona hakuna cha kumzuia na kwa sasa umemuingia kwenye damu.

“Nimebahatika kushinda Mataji zaidi ya 20 katika mashindano mbalimbali, ndoto zangu ni kuhakikisha nafanya vizuri kimataifa, ndio maana nafanya mazoezi kwa bidii, ili kuzitafsiri ndoto kuwa kwenye vitendo,” anasema.

Anasema kabla ya kutani kuingia kwenye upro, anatamani kuona anatoa mchango kwenye timu ya taifa kunyakua mataji mbalimbali, “Miaka ya baadaye nitamani natamani kutani ili niwe pro na uzuri wa huu mchezo ukifanya mazoezi bila kutegea hauna upendeleo, hivyo ni rahisi kuishi ndoto zako.”

Anasema gofu ni mchezo unaoongoza kwa upendo na kujenga familia haubagui unacheza na mtu gani; “Unaweza ukacheza na babu, baba, mke, watoto ili mradi tu wajue sheria zake, ila mingine ambayo mtu akifikia umri fulani inakuwa ngumu kucheza tena,” anasema na kuongeza;

“Vijana tunaocheza gofu tuna nafasi ya kujifunza hekima, ustaarabu, maisha, utu, kwa sababu tunawakedi vijana na watu wazima ambao wameshaona mambo mengi, hivyo hakuna geni kwao kwenye ulimwengu huu, tunajikuta tunaepukana na akili mbaya za ujana.”

Tukio ambalo hatakaa alisahau wakati anacheza viwanjani anasimulia, “Kuna siku moja nilipiga shoti ikaenda moja kwa moja shimoni, kwani ni kitu kinachotokea kwa nadra kwa baadhi yetu, ingawa wapo wengine ambao hilo kwao ni kitu cha kawaida kabisa.”

Anawashauri wazazi kufumbua macho, kuwapa watoto wao nafasi ya kuchagua michezo wanayotaka, akiamini inaweza ikawapa mafanikio ya maisha yao.

“Kitu kinachonifurahisha ni kuona Chama Cha Gofu Tanzania (TGU) kinachoongozwa na Rais Gilman Kisiga kina mpango wa kuhakikisha gofu inafundishwa mashuleni, wanafunzi wanaoupenda watapata nafasi ya kujifunza,” anasema na kuongeza;

“Gofu hauzuii wanafunzi kuendelea na masomo yao, tena itakuwa rahisi kwao kupitia mchezo huo kukutana na watu wa kuwaajiri kutokana na fani walizozisomea.”