Kwa Yanga hii mtateseka sana, Mbrazil naye ndani

TANGA. MASHABIKI wa Yanga wakiwa na furaha jana walishangilia ushindi wa mabao 2-0 waliopata dhidi ya Coastal Union kwa kuimba kwa kuuliza...’Kwani bado nani...?

Mabao mawili, moja kila kipindi yaliyofungwa na Fiston Mayele na Saido Ntibazonkiza yaliiwezesha Yanga kukata mzizi wa fitina mbele ya Coastal Union katika pambano kali lililopigwa kwenye uwanja uliojaa mabonde kama matuta ya viazi wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Ushindi wa jana ni wa 10 katika mechi 12 za Ligi Kuu msimu huu, huku pia Yanga imetimiza jumla ya mechi 19 bila kupoteza tangu ilipofungwa mara ya mwisho Aprili 25 mwaka jana na Azam.

Coastal imekuwa ikiitesa sana Yanga kwenye uwanja huo ikiwamo msimu uliopita ilipowafumua wababe hao wa Jangwani mabao 2-1 na kuwatibulia rekodi yao ya kucheza mechi 32 mfululizo bila kupoteza.

Mchezo wa jana uliokuwa na ahadi za mamilioni ya fedha kwa nyota wa timu zote kama wangeibuka na ushindi na turufu ikaiangukia Yanga iliyoibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika pambano kali lililojaza mashabiki uwanjani.

Coastal iliahidi kuwapa nyota wake Sh50 milioni zilizotokana na ahadi za wadau wake akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, AdamMalima, huku Yanga kabla ya mechi hiyo walipewa Sh20 milioni na kwa ushindi huo wameongezewa Sh50 milioni.

Ushindi huo wa jana umeifanya Yanga kufikisha pointi 32 na mabao 22 ya kufunga, huku Coastal ikisaliwa na alama zao 17 katika nafasi ya nne baada ya mechi 12.

Katika mchezo huo, Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alianzisha mziki mnene wakiwamo nyota wake wa kimataifa waliokosekana kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambako ilitema ubingwa wake uliobebwa na Simba, akiwamo Djuma Shaban na Khalid Aucho.

Coastal nayo ikiwa na rekodi tamu ya kuitesa Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani, ilianza kwa kasi na kukosa bao dakika ya 4 tu, baada ya shuti la Benedicto Jacob kuokolewa na beki Dickson Job na kuwa kona iliyokosa madhara.

Yanga ilijibua mapigo ikinufaika na makosa ya mabeki wa Coastal pasi fupi ya Mtenje Juma ilinaswa na Fiston Mayele lakini shuti lake lilisukumwa na kipa Mussa Mbisa nje kidogo ya lango lakini waamuzi hawakuona kama ilipaswa kuwa kona.

Timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu na dakika ya 41, Mayele alifunga bao tamu la kichwa akimalizia krosi yenye macho kutoka kwa beki Djuma Shaban.

Djuma alipiga mpira huo baada ya kupokea pasi murua ya Saido ambaye jana aliupiga mwingi, huku akiwa na vita nzito na nahodha wa Coastal Juma Ntenje.

Hilo lilikuwa bao la sita kwa Mayele msimu huu na kuongoza orodha ya wafungaji wa ligi hiyo.

Ubovu wa uwanja ulimnyima Saido bao alipokimbia na mpira upande wa kushoto lakini wakati akijindaa kuupiga ukadunda mbele yake na kupaisha nafasi ambayo ilionekana angefunga kirahisi.

Muda wote wa mchezo wachezaji wa timu zote mbili walionekana kuhangaika kumiliki mpira au kupiga pasi sahihi kutokana na uwanja kuwa na miinuko na mabonde mengi,

Kipindi cha pili pili wenyeji walirudi kwa kufanya mabadiliko wakimtoa Semtawa nafasi yake ikichukuliwa na Japhet Vedastus na kuongeza kasi ya mchezo wao kutafuta bao la kusawazisha, lakini umakini wa kipa Abuutwalib Mshery na mabeki wake wakiongozwa na nahodha Bakar Mwamnyeto iliwanyima nafasi hiyo.

Dakika ya 68 Coastal ilifanya mabadiliko mengine ikiwatoa Gustaph Saimon na Jacob na kuwaingiza Vincent Aboubakar na Haji Ugando.

Dakika ya 75 kipa Mshery aliokoa kishujaa mpira wa kichwa cha Victor Akpan akimalizia krosi ya Moubarack Amza katika shambulizi la mpira wa friikiki.

Yanga ilifanya mabadiliko mawili dakika ya 78 kwa kuwatoa Moloko na Feisal Salum na kuwaingiza Dickson Ambundo na Farid Mussa, huku Coastal nayo katika ya 85 ikamtoa tena Victor Akpan na kumuingiza Ambrose Mganda na Yanga nao wanafanya mabadiliko dakika ya 86 ikimtoa Mayele aliyepata maumivu akiingia Heritier Makambo.

Wakati mashabiki wakiamini mechi imeisha kwa bao moja, Saido aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 90 na la nne kwake kwa shuti kali akimalizia pasi safi ya Farid.


COASTAL: Mbissa, Mbarouk, Shiga, Kyata, Athuman, Mtenje, Akpan/Ambrose, Sopu, Jacob/Ugando, Semtawa na Gustaph/Vincent

YANGA: Mshery, Djuma, Yassin, Job, Mwamnyeto, Bangala, Moloko/Ambundo, Aucho, Mayele/Makambo, Feisal/Farid, Saido