Mayele amtingisha kocha Mmarekani

Saturday January 15 2022
Mayele PIC
By Daudi Elibahati

KIKOSI cha Yanga tayari kimetua mkoani Tanga kwa ajili ya mechi yao ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union itakayopigwa wikiendi hii, huku kocha anayewanoa Wagosi wa Kaya, Melis Medo akikiri mziki wa straika Fiston Mayele sio mchezo ila wamejipanga kumdhibiti.

Mayele ni kati ya wafungaji vinara wa mabao wa Ligi Kuu akiwa na mabao matano kama Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania, Jeremiah Juma wa Prisons, George Mpole wa Geita Gold na Reliants Lusajo wa Namungo.

Kocha Medo ambaye ni raia wa Marekani, alisema amejipanga na vijana wake ili kukabiliana na straika huyo wa Yanga, ili asiwatie njaa kama alivyofanya kwa timu kadhaa alizokoutana nazo.

“Namjua Mayele ni mchezaji mzuri sana, anajituma uwanjani na ana njaa ya mabao, lakini nasi tumeanza mapema kujiandaa kumdhibiti yeye na nyota wengine wa Yanga, ili tumalize dakika 90 tukiwa wababe uwanja wa nyumbani,” alisema Medo na kuongeza;

“Siiogopi Yanga, ila naiheshimu kwani ni timu yenye wachezaji bora, nimekiandaa vyema kikosi changu kuikabili na kuhakikisha tunapata matokeo mazuri, kwani tulipoteza katika mechi yetu ya mwisho tukiwa nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar.”

Yanga itaifuata Coastal katika mechi inayowakumbushia machungu waliyokutana nao msimu uliopita ikiwa kinara wa ligi bila kupoteza na kucharazwa mabao 2-1, kwani hata sasa ndio inayoongoza msimamo, ikiwa pia haijapoteza katika mechi zao 11 ilizocheza msimu huu.

Advertisement

Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 29, huku Coastal ikiwa nafasi ya nne na alama zao 17 kila moja ikicheza mechi 11.

Katika mechi yao ya msimu uliopita iliyopigwa Machi 4, 2021 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Yanga ilitibuliwa rekodi ya kucheza mechi 32 mfululizo za ligi bila kupoteza. Kwa sasa Yanga imecheza mechi 18 bila kupoteza tangu ilipolala mara ya mwisho na Azam April 25, 2021.


Advertisement