Kumbe dili la Sancho Manchester United tangu Machi

Muktasari:
Katika mkutano huo, moja kati ya mazungumzo yalikuwa Sancho kwenda kukipiga Old Trafford, lakini kwa wakati huo mambo yalikwama kwa sababu mchezaji mwenyewe hakuwa tayari kuondoka kwenye timu.
MANCHESTER, ENGLAND. STAA Mwingereza, Jadon Sancho amekuwa hakauki kuhusishwa na mpango wa kutua Manchester United huku ikiwa imefichuka mazungumzo ya kiungo huyo wa Borussia Dortmund kutua Old Trafford yalianza tangu Machi mwaka huu.
Mabosi wa Borussia Dortmund chuko nyuma iliwahi kusema kuhusu maombi inayopata kutoka kwenye klabu moja kubwa inayohitaji saini ya mchezaji huyo aliyekuwa akikipiga Manchester City utotoni.
Mkurugenzi wa Michezo wa Dortmund, Michael Zorc alithibitisha amekutana na mabosi wa Man United Machi, ambapo mkutano huo ulikuwa na mabosi wengine wa klabu kama Matthias Sammer, Sebastian Kehl na Mwenyekiti Hans-Joachim Watzke.
Katika mkutano huo, moja kati ya mazungumzo yalikuwa Sancho kwenda kukipiga Old Trafford, lakini kwa wakati huo mambo yalikwama kwa sababu mchezaji mwenyewe hakuwa tayari kuondoka kwenye timu.
Zorc alisema: "Mada moto ya sasa ni Sancho na Manchester United. Ndio mjadala uliopo kwa sasa kwenye timu na washauri wake. Vikao vilifanyika na Man United ilileta washauri wake. Lakini ninachokifahamu ni kwamba mshauri wa klabu aliwaambia kwa ofa yoyote ya pesa ambayo Man United itatoa, Sancho hawezi kuruhusiwa kuondoka kwenye majira ya kiangazi ya mwaka huu.
Mchezaji mwenyewe pia hakuwa tayari kuhama kwenye majira haya ya kiangazi."
Sancho bado yupo kwenye rada za Man United na Kocha Ole Gunnar Solskjaer ni shabiki mkubwa wa winga huyo Mwingereza.
Hata hivyo, kumekuwa na ripoti Sancho amekubali kusaini dili jipya huko Dortmund, ambalo litamshuhudia akiweka mfukoni Pauni 10 milioni kwa mwaka.