Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Rwanda atamani kibarua cha Taoussi Azam

RWANDA Pict

Muktasari:

  • Seninga amesema amekuwa akiifuatilia Ligi Kuu Bara ambavyo inapanda katika viwango vya soka vya Afrika ikishika nafasi ya 5 kwa mujibu wa CAF na amehamasishwa na kile ambacho kimefanywa na Yanga na Simba ambazo zimecheza fainali za Kombe la Shirikisho Afrika ndani ya misimu mitatu hii.

MAFANIKIO ya Simba na Yanga na Ligi Kuu Bara kwa ujumla katika ngazi ya kimataifa, yamempa wivu kocha mwenye uzoefu kutoka Rwanda, Innocent Seninga, akisema anatamani kuja kufanya kazi katika ligi hiyo.

Seninga amesema amekuwa akiifuatilia Ligi Kuu Bara ambavyo inapanda katika viwango vya soka vya Afrika ikishika nafasi ya 5 kwa mujibu wa CAF na amehamasishwa na kile ambacho kimefanywa na Yanga na Simba ambazo zimecheza fainali za Kombe la Shirikisho Afrika ndani ya misimu mitatu hii.

Amezitaja pia timu nyingine ambazo zinafanya vizuri ikiwamo Singida Black Stars ambayo msimu ujao itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na Azam FC.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Kigali, Rwanda kocha huyo alisema: “Timu za Tanzania zinafanya vyema sana. Azam FC, kwa mfano, ni klabu ninayoiheshimu sana. Ni kati ya timu ambazo nikipewa ofa siwezi kukataa. Ni klabu yenye ndoto kubwa, mazingira ya kisasa ya kazi na yenye utulivu. Hayo ndiyo mambo ambayo kocha yeyote anayahitaji kufanya kazi kwa ufanisi.”

Huku klabu ya Azam ikiwa kwenye hatua za tathmini ya mustakabali wa benchi lake la ufundi kufuatia mkataba wa kocha Rachid Taoussi kumalizika mwishoni mwa msimu huu, Seninga anaamini, Azam ni klabu yenye nafasi kubwa ya kutawala soka la Afrika Mashariki na kutisha Afrika kwa ujumla.

Kocha huyo ambaye kwa sasa yupo huru baada ya kumaliza mkataba na Etincelles FC ya Rwanda, ana historia ndefu ya mafanikio katika soka la Afrika Mashariki. Alipata umaarufu mkubwa akiwa na Police FC ya Rwanda msimu wa 2016/17 alipoifikisha nafasi ya pili kwenye ligi, huku akimkuza mfungaji bora wa msimu huo.

Pia amewahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Rwanda ‘Amavubi’ kwa vipindi tofauti kati ya mwaka 2018 hadi 2023.

Katika upande wa taaluma, Seninga amehitimu Shahada ya Elimu ya Michezo kutoka Kigali Institute of Education, na baadaye kupata diploma ya juu ya ukocha kutoka Chuo KiKuu cha Leipzig nchini Ujerumani.

Ana leseni ya CAF A, ikiwa ni kiwango cha juu kabisa kwa ukocha wa bara Afrika. Aidha, amepewa majukumu mbalimbali ya kufundisha makocha barani Afrika kupitia CAF.

Mbali na kuwa kocha wa klabu kadhaa za Rwanda, kama vile Sunrise, Musanze, Bugesera na Etincelles, Seninga pia amekuwa sehemu ya maendeleo ya wachezaji waliokuja kuwa nyota wa kimataifa akiwamo Danny Usengimana aliyewahi kucheza Tanzania na Misri, Biramahire Abeddy aliyecheza Tunisia, na Mico Justin aliyecheza Kenya.

Seninga anaongea lugha tano Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili, Kinyarwanda, na Kijerumani jambo ambalo humpa faida kubwa katika mawasiliano na wachezaji wa mataifa mbalimbali katika kazi zake.

Azam inaelezwa ipo mbioni kuachana na Taoussi aliyetua kuziba nafasi iliyoachwa na Youssouf Dabo, huku jina la Florent Ibenge na wengineo yakihusishwa.