Kocha mpya Simba aiwahi ASEC Mimosas

SIMBA wapo hatua ya mwisho za kumtangaza Kocha mpya kabla ya mechi yao ya kwanza dhidi ya ASEC Mimomas itakayochezwa Jumamosi, kwenye uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Tayari Abdelhak Benchikha, raia wa Algeria jina lake limepigwa chini na mpaka jana jioni Simba ilikuwa kwenye harakati za kumalizana na Mtunisia Radhi Jaidi.

Simba itacheza na ASEC nyumbani ikiwa na nyota wote wakiwemo wale waliokuwa kwenye timu za Taifa zilizoshiriki mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 ambao ni Henock Inonga ambaye timu yake ilimaliza juzi, Clatous Chama atakayejiunga na timu Alhamisi akitokea Morocco timu yake ikicheza na Niger.

Wachezaji ambao wako Taifa Stars ni Aishi Manula na Kibu Denis watajiunga na wenzao baada ya Stars kumaliza mechi na Moroco itakayochezwa leo Jumanne usiku.

Simba ambayo ipo Kundi B pamoja na timu ya Jwaneng Galaxy, Asec Mimosas na Wydad Athletic, imeelezwa kuwa baada ya kumaliza mechi hiyo, Simba itaondoka kwenye Botswana kucheza na Jwaneng na kuunganisha nchini Morocco kucheza na Wydad.

Simba kwa sasa inaongozwa na Daniel Cadena pamoja na Seleman Matola ambao watasimamia mechi hiyo na endapo kocha huyo anayetarajiwa kutangazwa muda wowote kuanzia sasa atakuwa tayari akifuatilia mwenendo wa wachezaji.


Cadena, Matola kufanya tathimini

Wiki hii Simba inaonekana kuwa kimkakati zaidi ambapo viongozi wa timu hiyo kumtangaza kocha, kuutaka ushindi dhidi ya Asec Mimomas lakini wakiwapa majukumu mazito makocha wao Mhispaniola Cadena na Matola.

Uongozi umewapa kazi Cadena na Matola ya kuaandaa ripoti ya kikosi hicho ikiwemo kupendekeza wachezaji wa kuachwa kwani Simba imepania kufanya usafi kwenye dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Disemba 16, mwaka huu, kwa kuacha baadhi ya nyota wake na kushusha majembe mapya.

“Ishu ya kocha bado ina ka’ugumu flani hivi. Sasa hatuwezi kuendelea kusubiri kocha aje ndio tufanye vizuri, tumewaagiza makocha waliopo (Cadena na Matola), kutengeneza mpango wao na kujiamini kwani wao ndio watakuwa kwenye benchi katika mechi ijayo na Asec.

“Tumefanya hivyo kwakuwa hatutaki kukurupuka, na wakati Cadena na Matola wakiendelea na mipango ya mechi pia tumewaomba watuandalie ripoti ya kikosi chetu ili kocha mpya akija aipitie na aongeze au kupunguza baadhi ya mambo kabla dilisha dogo halijafunguliwa,” alisema mmoja ya wakurugenzi wa Bodi ya Simba (jina tunalo).

Majina ya Jaidi na Benchikha ndio yapo mezani kwa Simba yakijadiliwa na sababu kubwa ya kuchelewesha maamuzi ya nani akabidhiwe timu ni makocha wawili hao kuhitaji mkwanja mrefu.