Kocha Mkenya kwenye nyayo za Simba

Muktasari:
- Uamuzi wa Simba umefikiwa muda mfupi baada ya kuelezwa kuwa upo kwenye mpango wa kuachana na Kocha Mkuu, Yussif Basigi kutokana na kushindwa kufikia malengo.
UONGOZI wa Simba upo kwenye mchakato wa kumalizana na Kocha wa timu ya taifa ya Kenya ya wanawake Harambee Starlets, Beldine Odemba kwa ajili ya kuinoa Simba Queens msimu ujao.
Uamuzi wa Simba umefikiwa muda mfupi baada ya kuelezwa kuwa upo kwenye mpango wa kuachana na Kocha Mkuu, Yussif Basigi kutokana na kushindwa kufikia malengo.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeiambia Mwanaspoti kuwa mchakato wa mazungumzo kwa ajili ya kumpata kocha huyo unaendelea vizuri na wanafanya kwa ukaribu baada ya kuja Tanzania na timu yake kwenye michuano ya Cecafa.
“Bado hatujamalizana na Basigi hadi hapo tutakapotoa taarifa, ila mchakato wa kutafuta kocha unaendelea mambo yakiwa tayari mtafahamishwa,” amesema mtoa taarifa huyo na kuongeza:
“Juu ya mazungumzo na kocha Odemba ni mapema sana kuzungumzia hilo, lakini ni kweli mazungumzo ya kumuhitaji kwa ajili ya kuja kuinoa Simba Queens msimu ujao yapo lakini mimi sio mzungumzaji sahihi.”
Odemba yupo nchini Tanzania kwa ajili ya michuano ya Cecafa ambayo anaitumia kwa maandalizi ya mechi za kufuzu fainali za kombe la mataifa ya Africa (WAFCON) mwaka ujao nchini Morocco.
Timu yake ya taifa ya Kenya kesho Jumapili, Juni 15, itafungua dimba dhidi ya Burundi wakati Starlets itakabiliana na Gambia katika mechi ya kufuzu WAFCON, Septemba, mwaka huu.
Kuhusu Basiga ambaye alijiunga na Simba akitokea Hasacaas Ladies ya Ghana na ukiwa ni msimu wake wa kwanza kwenye ligi, amepoteza mchezo mmoja dhidi ya Yanga Princess na sare dhidi ya JKT akishinda 12.
Basigi alichukua mikoba ya Juma Mgunda aliyebeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara (WPL) msimu juzi bila kupoteza mchezo akiifunga Yanga na JKT nyumbani na ugenini kabla ya kutimkia Namungo.