Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Bora kaa la moto

Muktasari:

Ukifuatilia kwa umakini kuna kitu huwa kinawapata makocha wanaobahatika kupata tuzo hiyo hapa nchini. Nami najiuliza tatizo huwa ni nini? Wachezaji au kulikoni nifuate kidogo ujue nini namaanisha:

IMEKUWA ni kama utamaduni kwa wasimamizi wa ligi duniani kutoa zawadi kwa makundi tofauti yanayoshiriki ligi hizo.

Kwa hapa nchini ukiacha msimu huu waliokuwa wadhamini wa Ligi Kampuni ya Simu ya Vodacom ilikuwa ikitoa zawadi kwa Kipa Bora, Mfungaji Bora, Mchezaji Bora, Timu Yenye Nidhamu, Mwamuzi Bora na Kocha Bora achilia zawadi kwa washindi wa kwanza hadi wa nne.

Ukifuatilia kwa umakini kuna kitu huwa kinawapata makocha wanaobahatika kupata tuzo hiyo hapa nchini. Nami najiuliza tatizo huwa ni nini? Wachezaji au kulikoni nifuate kidogo ujue nini namaanisha:

1. JUMA MWAMBUSI- 2013/ 2014

Nani asiyeukumbuka msimu huu uliokuwa bora kwa kocha wa kikosi cha Mbeya City, Juma Mwambuzi kilichomaliza msimu kikishika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga iliyoongozwa na Azam iliyokuwa bingwa kwa mara ya kwanza.

Kocha Mwambusi ambaye msimu wa 2007 alijiunga na kikosi cha Tanzania Prisons akitokea Arusha kumsaidia aliyekuwa kocha wa mfano wake Marehemu Juma Kalomba kunako timu ya Pallsons. Mwambusi aliisaidia Prisons kufanya vizuri na kumaliza nafasi ya pili kisha kupata uwakilishi wa kitaifa

Baadaye Mwambusi alichukuliwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuinoa Mbeya City na kuipandisha Ligi Kuu. Msimu wake wa kwanza Mbeya City ilikuwa moto ikitembeza vipigo nyumbani na ugenini na kumaliza Ligi Kuu kwenye nafasi ya tatu juu ya Simba.

Msimu uliofuata Mbeya City ambayo iliondokewa na wachezaji wake wachache haikuwa ile tuliyoizoea. Kulikuwa na mgogoro wa chini kwa chini kwa wachezaji kucheza chini ya kiwango huku wakipata sapoti ya kocha kwa madai ya kudai haki zake.

Hii ilisababisha timu kufanya vibaya ikiwa chini ya msimamo wa ligi kwa muda mrefu na kumfanya Kocha Mwambusi kuondoka na akipata ofa nzuri Klabu ya Yanga.

2. MBWANA MAKATA - 2014/ 2015

Mbwana Makata alikuwa kocha bora wa msimu huo alipoifundisha Prisons ya Mbeya ambayo mwanzoni mwa msimu haikuwa kwenye hali nzuri ikifungwa michezo mingi na kushindwa kupanda juu ya msimamo wa ligi.

Ndipo uongozi wa Tanzania Prisons ulipomchukua kocha huyo na kazi aliyofanya ni kuibakisha timu Ligi Kuu huku ikipanda hadi nafasi za juu mwishoni mwa msimu!

Makata alipata nafasi ya kuwa kocha bora wa msimu akimzidi Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm ambaye aliisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kitu ambacho kilizua maswali mengi.

Msimu wa 2014/ 2015 Makata alihamia Kagera Sugar. Unaweza kusema Alianza vibaya ligi labda kwa sababu timu yake ilikuwa haitumii uwanja wake wa nyumbani asilia wa Kaitaba ambao ulikuwa kwenye matengenezo na kutumia viwanja vya Kambarage na Kirumba, huko ndiko Kocha Makata alikopotea baada ya kushuhudia Kagera Sugar ikisota kwa muda mrefu chini ya msimamo wa Ligi Kuu na almanusura iteremke daraja.

Ndipo uongozi wa Kagera Sugar ulipoachana rasmi na kocha huyo na kumchukua mwingine wa muda.

3. HANS PLUIJM - 2015/ 2016

Wadau wengi wa soka walitegemea kabisa kumuona kocha huyo aliyeipa ubingwa klabu ya Yanga msimu wa 2014/ 2015 ikiuchukua ubingwa huo mikononi mwa Azam waliokuwa mabingwa, Pluijm aliifanya Yanga kucheza kwa uelewano na kuchukua ubingwa kirahisi.

Msimu uliofuata wa 2015/2016 ulikuwa bora kwa kocha huyo, huu ndio ambao licha ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu kwa idadi kubwa ya pointi na mabao mengi, timu yake ilizoa tuzo nyingi kuanzia ile ya mchezaji bora hadi mshambuliaji bora.

Pamoja na kuchukua ubingwa kocha huyo aliiwezesha Yanga kushiriki kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika huku pia akifanikiwa kuchukua ubingwa wa Kombe la ASFC.

Hakuna shaka ubora wa Pluijm haukutakiwa kupingwa wala kuulizwa zaidi ya kupewa ushirikiano kufuatia kubeba tuzo hiyo. Ni kama vile tuzo hiyo ina warakini baada ya klabu yake kuingia mkataba na Kocha Mzambia, George Lwandamina bila ya yeye kujua na baadaye kupandishwa cheo na kuwa mkurugenzi wa ufundi wa Yanga nafasi ambayo yeye binafsi hakuipenda. Kitu hicho kilimfanya kwenda kuifundisha timu nyingine kwenye Ligi Kuu ya Singida United.

Alipotua Singida United. Pluijm alitarajiwa kufanya mambo makubwa lakini matokeo yake yamekuwa tofauti na sasa ametua Azam FC.

4. MECKY MAXIME - 2016/ 2017

Ulikuwa msimu bora kwa kocha huyu kijana aliyeitumikia Mtibwa Sugar kama mchezaji na kama kiongozi ndani ya timu hiyo na ile ya taifa, Mecky alicheza kwa uaminifu na nidhamu ya hali ya juu na kuingia kwenye eneo la ufundi.

Akiwa na Kagera Sugar, Mecky aliiwezesha kucheza soka zuri lililojaa ushindani wa hali ya juu. Inakumbukwa msimu huo timu hiyo iliipunguza Simba makali yake ya ya kuukaribia ubingwa wa Ligi Kuu msimu huo!

Huo ndio msimu ambao Kagera Sugar ilipovamia nafasi za juu kwenye Ligi Kuu na kukaa juu ikiishusha Azam na kutoa mmoja kati ya vijana waliogombania tuzo ya ufungaji bora, Mbaraka Yussuf.

Msimu uliofuata wa 2017/ 2018 Kagera Sugar ilitumia muda mrefu kujinasua kutoka chini ya msimamo wa ligi na kuna kipindi ilikuwa chini kabisa. Licha ya soka la timu hiyo kutobadilika bado ilikuwa ikihangaika kupata ushindi. Hii ndio dalili ya wale makocha wanaochukua tuzo ya kocha bora kuhangaika msimu unaofuata au vipi? Mwisho wa msimu tulishuhudia kocha huyo akifanikiwa kuibakiza timu yake Ligi Luu.

5. ABDALLAH JUMA `BARES` - 2017/ 2018

Kocha huyu aliyeichukua Tanzania Prisons katikati ya msimu wa mwaka juzi na kusaidia kuibadilisha kutoka kwenye ushiriki angalau kuirudisha kule ilikokuwa misimu kadhaa nyuma ile ya 1998 - 2008 .

Kocha Abdallah Juma aliifanya timu hiyo kuwa tishio kwenye Ligi Kuu katika msimu huo tofauti na matarajio ya wengi.

Kikubwa Kocha Juma alifanikiwa kuifanya timu yake kuwa na nguvu na kumudu kucheza mipira mirefu.

Alifanikiwa kuifanya kazi hiyo kwa ufasaha na akienda tofauti kabisa na utamaduni wa makocha wengi wanaotoka Zanzibar na kuingia Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambao wengi wanaotumia sana pasi nyingi fupi fupi .

Kingine kocha huyo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kujenga eneo la ulinzi lenye wachezaji wanaojituma sana kina Jumanne Elfadhili, Nurdin Chona , Salum Kimenya, Laurian Mpalire na James Mwasote.

Prisons alionekana kucheza soka la nguvu na uelewano mkubwa mwisho wa msimu, miamba hiyo ya Mbeya ilimaliza kwenye nafasi ya nne za juu. Ni hatua kubwa kufikiwa na timu hiyo baada ya muda mrefu.

Sasa hali imekuwa tofauti tangu Ligi Kuu ilipoanza. Pamoja na kuweka kambi ya muda mrefu kule Zanzibar, Prisons inaonekana kuhangaika mno kupata matokeo tofauti na ilivyo kawaida yake ya msimu uliopita.

Bado timu hiyo chini ya kocha bora wa Ligi Kuu wa msimu uliopita. Na hali imekuwa tofauti huku kocha na benchi lake la ufundi wakihangaika bila ya kujua cha kufanya. Hebu tuangalie tuzo bora ya ukocha Tanzania itaendelea kumtesa Kocha Abdalah Juma msimu huu?