KO ya Mama imefichua ukweli

Muktasari:
- Knockout ya Mama ndiyo michuano ya funga mwaka kwa mchezo wa ngumi za kulipwa na pia ni ushuhuda kwamba ndondi ni mchezo wa pili kupendwa nchini na wenye kulipa vyema.
NGUMI za kulipwa ndio mchezo ulioifuatia soka kwa ubora mwaka 2024, na wadau wa michezo wanahofu michezo mingine kuendelea kudorora wakati soka ikidaiwa itazidi kuongoza kwa kutoa ajira 2025.
Knockout ya Mama ndiyo michuano ya funga mwaka kwa mchezo wa ngumi za kulipwa na pia ni ushuhuda kwamba ndondi ni mchezo wa pili kupendwa nchini na wenye kulipa vyema.
Kumekuwepo na mapambano mengi ya ndondi kwa miaka ya karibuni ambayo yamekuja kwa majina mbalimbali kama Vitasa na Rumble in Dar, na yote hayo na mengine mengi yaliyofanyika yamezifanya ngumi za kulipwa kuwa ni moja ya michezo inayolipa vyema washindi.
Kwa upande wa gofu, Lina PG Tour iliongoza kwani ilitoa Sh250 milioni kwa washindi 10 wa gofu ya kulipwa na ridhaa.
Bado mchezo huo haujaweza kuifikia soka kwa ajira nono, lakini angalau umekuwa na tija fulani kwa washindi.
Katika soka, Tanzania imefanya mengi makubwa kwa klabu na timu za taifa za wanaume na wanawake, wakati hali ya michezo mingine haikuwa na mafanikio makubwa, ikizingatiwa kwamba siku za nyuma ilikuwa na mashabiki wengi katika netiboli, riadha, magongo, vinyoya, mpira wa meza, skwashi, mpira wa mikono, wavu na raga.
Idd Mhunzi, mmoja wa walimu wa riadha jijini Dar es Salaam amedai michezo mingi inadorora kwa sababu inakosa watazamaji, hali ambayo inasababisha timu kukosa kipato na udhamini.
“Kifupi michezo ambayo haina washabiki inakosa watazamaji, viingilio na wadhamini na mwisho haitamlipa chochote mchezaji,” alisema Mhunzi.
Akiongeza, mcheza soka mkongwe nchini, Kaingilila Maufi alisema soka inalipa vizuri kwa sababu inatengeneza tija.
“Mcheza soka anayetumikia moja ya klabu kubwa ya Ligi Kuu anaweza kulipwa hadi Sh20 milioni kwa mwezi na wa chini anaweza kulipwa hadi Sh1 milioni. Hali hii inaifanya soka kuwa mchezo unaongoza kwa ajira,” alisema Maufi ambaye sasa anachezea Mshikamano Veterans ya Mbezi, Dar es Salaam.
Akifafanua zaidi kuhusu riadha, Mhunzi alisema kwa mbio ndefu za kilomita 42 na 21 zinatoa malipo ya hadi Sh2 milioni kwa washindi, lakini mwaka 2024 hakukuwa na mbio nyingi za marathoni kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Alisema riadha mwaka jana haikufanya vizuri kimataifa kama ilivyokuwa 2023 ambapo wanaridha kama Alphonce Simbu na Gabriel Geay walifanya vizuri. “Mwanariadha anaweza kulipwa hata Dola 50,000 kwa kushinda mashindano makubwa kama Golden na Diamond League, lakini Watanzania wengi hawalielewi hili,” alisema Mhunzi.