Kiungo Yanga arejea mchangani kiroho safi

Muktasari:
Katika mchezo huo ambao ulikuwa wa ufunguzi wa ligi hiyo kumsaka bingwa wa Mkoa wa Mwanza, Machinga FC ndio walitangulia kupata bao dakika ya 33 kupitia kwa Baraka David,bao lililosawazishwa na Leonard Alex dakika ya 90.
MWANZA. UNAMKUMBUKA Kiungo wa zamani wa Yanga, Emanuel Swita aliyewahi kutamba miaka hiyo? Sasa jamaa huyo kwa sasa anakipiga Ligi ya Mkoa wa Mwanza na jana aliisaidia timu yake Copco Veteran kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Machinga FC katika hatua ya 10 bora.
Nyota huyo ambaye na ailiichezea Toto Africans kipindi ikiwa Ligi Kuu, amekipiga pia klabu za Polisi Mara (Biashara United), Buseresere FC na sasa ameibukia timu ya Copco Veteran inayoshiriki Daraja la tatu Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mchezo wao wa Ligi ya Mkoa hatua ya 10 bora iliyoanza kurindima juzi, Swita alisema kuwa ameamua kukipiga huko wakati akisubiri Ligi kuu iishe ili asake timu mpya.
Alisema kuwa bado anaamini uwezo wake upo juu na kwamba malengo yake ni kuipa ubingwa wa Mkoa timu yake hiyo kisha atimke zake kwenye Ligi kuu au Daraja la kwanza msimu ujao.
“Bado naweza kucheza timu yoyote nimeamua kuwa huku kwa muda wakati nikisubiri Ligi Kuu iishe ili nisake timu ya kuchezea au ya daraja la kwanza,lakini nataka hii Copco niiachie ubingwa wa Mkoa,” alisema Swita.
Kwa upande wake Kocha wa Copco Veteran, Faisari How alisema kuwa ameamua kumleta kikosini mkongwe huyo ili kuongeza hamasa kwenye timu yake katika vita ya kusaka ubingwa wa Mkoa.
“Anaupiga mwingi na wala hajazeeka, nimemleta ili aongeze hamasa kwa wachezaji wengine na leo (jana) umeona alivyopambana tukasawazisha bao kwa hiyo ninaamini mchango wake utaonekana,” alisema How.
Katika mchezo huo ambao ulikuwa wa ufunguzi wa ligi hiyo kumsaka bingwa wa Mkoa wa Mwanza, Machinga FC ndio walitangulia kupata bao dakika ya 33 kupitia kwa Baraka David,bao lililosawazishwa na Leonard Alex dakika ya 90.