Prime
Yanga, Bodi ya Ligi waachana njia panda!

Muktasari:
- Kupokonywa pointi tatu hadi 15 pamoja na faini ni adhabu ambayo huenda Yanga ikakutana nayo iwapo haitofika uwanjani Juni 15.
Dar es Salaam. Licha ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutangaza tarehe mpya ya kuchezwa mechi ya marudiano kati ya Yanga na Simba, hali ya sintofahamu imeendelea kutanda upande wa Jangwani kuhusu hatma ya mchezo huo wa Kariakoo Dabi.

Katika taarifa yao ya hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii, Yanga wameonyesha ratiba ya mechi zao tatu tu zilizobaki msimu huu ambapo mechi mbili ni za Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons itakayochezwa Juni 18, ugenini na Dodoma Jiji ambapo Yanga itakuwa nyumbani Juni 22 pamoja na mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Singida Black Stars ambao bado haujapangiwa tarehe lakini mechi ya Dabi haijawekwa kwenye ratiba yao.

Mchezo huo namba 184 wa raundi ya pili ya Ligi Kuu, ambao awali ulipangwa kuchezwa Machi 8, 2025, uliahirishwa baada ya Simba kudai kuzuiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa siku moja kabla ya mechi ikiwa kama timu mgeni. Tukio hilo lilizua mtafaruku mkubwa kuelekea mechi hiyo ambapo Bodi ya Ligi Kuu ilitangaza kuhairishwa kwa mchezo huo, huku Yanga wakitoa tamko kuwa hawatacheza tena mechi hiyo.
Yanga walipeleka malalamiko yao katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), wakitaka mechi hiyo isichezwe na wapatiwe pointi tatu, lakini shauri hilo halikufua dafu baada ya CAS kutupilia mbali ombi lao kwa kukosa mashiko ya kisheria.
Hivi karibuni, TPLB ilitangaza rasmi kwamba mechi hiyo ya Dabi sasa itapigwa Juni 15, 2025. Hata hivyo, hadi sasa Yanga hawajatoa tamko la wazi kuhusu kushiriki kwenye mechi hiyo, huku kukiwa na taarifa zinazothibitisha kuwa Klabu hiyo itakuwa na mechi ya kirafiki siku hiyo dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, jambo linalozidi kuzua maswali kuelekea katika mchezo wa dabi.

Wakati Simba wakiwa wameonyesha wapo tayari kwa mchezo huo, msimamo wa Yanga unaonekana kuwa uleule wa kutocheza na iwapo wataendelea kususia, huenda wakakabiliwa na adhabu kutoka kwa mamlaka za soka. Kupokonywa pointi tatu hadi 15 pamoja na faini ni adhabu ambayo huenda Yanga ikakutana nayo iwapo kama isipofika uwanjani Juni 15.