Joshua Mutale haamini kilichomkuta

Muktasari:
- Mutale ambaye ana asisti mbili Ligi Kuu pamoja na mabao manne yakiwamo matatu ya Kombe la FA na moja la Kombe la Shirikisho Afrika, aliliambia Mwanaspoti kuwa, ubora ulioanza kuuonyesha wakati ligi inaelekea mwishoni ndio umempa fursa ya kuonekana na timu ya taifa bila kutarajiwa.
WINGA wa Simba, Joshua Mutale amesema bado haamini kama kaitwa timu ya taifa ya Zambia 'Chipolopolo' inayojiandaa kucheza mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya Tunisia na Sudan, akisema kwake imekuwa kama ni muujiza na imempa nguvu kupambana zaidi.
Mutale ambaye ana asisti mbili Ligi Kuu pamoja na mabao manne yakiwamo matatu ya Kombe la FA na moja la Kombe la Shirikisho Afrika, aliliambia Mwanaspoti kuwa, ubora ulioanza kuuonyesha wakati ligi inaelekea mwishoni ndio umempa fursa ya kuonekana na timu ya taifa bila kutarajiwa.
"Nimefarijika na kupata nguvu ya kupambana baada ya kuitwa kuitumikia timu ya taifa ambayo ni ndoto ya kila mchezaji sina neno zaidi ya kuona ni Mungu tu," alisema Mutale na kuongeza;
"Mchezaji ambaye anapata nafasi katika timu ya taifa lake, CV yake inaongezeka na kuona anathaminiwa, binafsi nashukuru kupata fursa hiyo kati ya wachezaji wengi wanaocheza ndani na nje ya Zambia."
Alisema anakwenda kukutana na wachezaji ambao wanacheza ligi tofauti, hivyo atapata vitu vingi vya kiufundi, vitakavyoendelea kuimalisha kiwango chake:"Kukutana wachezaji ambao mnacheza maeneo tofauti kunasaidia kujifunza vitu vingi ikiwemo nidhamu."
Baada ya kukosa taji la Shirikisho, Simba imeelekeza macho kwenye ligi na Kombe la FA. Na baada ya kumalizana na Singida Black Stars katika mechi ya jana Jumatano, timu hizo mbili zinatarajiwa kukutana tena Mei 31 kwenye nusu fainali ya FA, mechi ambayo itakuwa fursa nyingine kwa Mutale kuonyesha kuwa moto wake hauzimiki kirahisi.
Mutale alipitia kipindi kigumu kilichojaa mashaka, akijikuta nje ya kikosi cha kwanza, huku baadhi ya mashabiki na wadau wakianza kuhoji ubora wake, lakini haikuwa sababu ya kuporomoka zaidi, badala yake, alijikuta akipata nguvu mpya kupitia imani ya kocha Fadlu Davids.
“Wapo mashabiki ambao walikuwa wananitia moyo hata nilipokuwa napitia wakati mgumu. Kocha Fadlu (Davids) na benchi lote la ufundi hawakuwahi kunikatia tamaa. Walinipa sababu ya kupigana, niliamini utafika wakati wangu,” alisema Mutale.
Mchezaji huyo ambaye amejifunga kwa mkataba na Simba hadi 2027, anaonekana sasa kuwa silaha muhimu kwa kocha Fadlu Davids.