Kiungo KenGold katika rada za Coastal Union

Muktasari:
- Mchezaji huyo amefunga bao moja kati ya 22 ambayo KenGold imeshinda, huku ikishika nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi ikiwa imecheza mechi 28 ikishinda tatu, sare saba na kupoteza 18.
KIUNGO Mkongomani wa KenGold, Kiala Lassa anadaiwa kutimkia Coastal Union ambako amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo.
Mchezaji huyo amefunga bao moja kati ya 22 ambayo KenGold imeshinda, huku ikishika nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi ikiwa imecheza mechi 28 ikishinda tatu, sare saba na kupoteza 18.
Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja wa viongozi wa Coastal Union ameliambia Mwanaspoti kuwa kiungo huyo ameshasaini mkataba na klabu hiyo.
"Tumeanza kusajili rasmi. Wapo mastaa ambao tumefanikiwa kuwapata na miongoni mwao ni Lassa ambaye ni matumaini yetu kuwa atakwenda kuongeza nguvu," alisema kiongozi huyo.
"Mipango yetu ni mikubwa na wanaosema kwamba hatuna pesa za kusajili tunawapa muda ili waje kuona kile tutakachokifanya msimu ujao."
Katika mahojiano maalumu na Mwanasapoti hivi karibu, kocha wa timu hiyo, Joseph Lazaro alikaririwa akiushauri uongozi kuboresha maeneo mawili kikosini ili msimu ujao ifanye vizuri katika ligi.
Lazaro alisema: "Kwa msimu ujao huwezi kubadili timu nzima, ila yapo maeneo makuu mawili hasa ya mbele ili kuwa na mwisho mzuri wenye matokeo (katika ligi). Eneo la viungo na washambuliaji linatakiwa kufanyiwa usajili. Tulipata tabu sehemu ya kwanza, kuna kufungwa na kufunga."
Lassa alianza kuichezea KenGold msimu huu akitokea DR Congo akiweka rekodi ya kufunga bao moja. Kwa sasa wachezaji wengi wa KenGold wameanza kusaka malisho mapya kwenye vikosi vingine baada ya timu hiyo kushuka daraja ikiwa na mechi mbili mkononi.